KAMATI YA MICHEZO ARUSHA YAKAMILISHA AWAMU YA KWANZA YA ZIARA YA VILABU

KAMATI YA MICHEZO ARUSHA YAKAMILISHA AWAMU YA KWANZA YA ZIARA YA VILABU

Na Joseph Ngilisho – Arusha

KAMATI ya Michezo Wilaya ya Arusha imekamilisha awamu ya kwanza ya ziara yake ya kutembelea vilabu na vyama vya michezo, ambapo mwitikio umekuwa mkubwa huku changamoto mbalimbali zikibainika.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mjumbe wa Kamati, Rashid Abdallah, alisema hatua hiyo imekuwa chachu ya kuimarisha mshikamano kati ya kamati na wadau wa michezo wilayani humo.

> “Tumemaliza awamu ya kwanza salama. Vilabu vimejitokeza kwa wingi, tumefahamu changamoto zao na sasa tunajiandaa namna ya kuzitatua ili michezo iendelee kukua Arusha,” alisema Abdallah.


Vilabu vilivyotembelewa ni pamoja na CTIDO, Nyota FC, IAA SC, Gymkhana, Jetkan’do Karate, Taekwondo, Arusha City SC, Polisi Morani SC, AFC Arusha pamoja na Chama cha Soka Wilaya ya Arusha Mjini (ADFA).

Lengo kuu la ziara hiyo lilikuwa ni kubaini changamoto zinazokabili vilabu na vyama vya michezo, ili kuanza kuzitafutia suluhu, hususan kuelekea maandalizi ya AFCON 2027 ambayo Tanzania ni mwenyeji mwenza.

Kwa upande wake, Katibu wa Kamati, ambaye pia ni Afisa Michezo wa Jiji la Arusha, Benson Maneno, alisema awamu ya pili ya ziara hiyo itaanza baada ya Septemba 29.

> “Kwa sasa tumepumzika ili kujiandaa kumpokea mwanariadha wa kimataifa Alphonce Simbu, ambaye ameweka historia kwa kutwaa medali ya dhahabu katika Mashindano ya Dunia 2025 yaliyofanyika Tokyo, Japan,” alisema Maneno.


Aidha, Abdallah alibainisha kuwa ripoti ya awamu ya kwanza itawasilishwa kwa Mwenyekiti wa Kamati ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, Joseph Mkude, kwa ajili ya utekelezaji wa maazimio hayo.

Ends...

Post a Comment

0 Comments