MGOMBEA URAIS AKACHA MKUTANO BAADA YA KUKUTA VITI TU VIKIMZAMA NA IDADI NDOGO YA WATU

By Arushadigital 

BAADHI ya wananchi mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, wamesikitishwa na kitendo cha mgombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama cha NCCR Mageuzi, Haji Ambari Khamisi kukacha kuwahutubia.



Wakizungumza baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Sabato mjini hapo, wamedai kwamba kitendo cha mgombea huyo kutohutubia kwa madai ya kukosa idadi kubwa ya watu si haki kwao.


Mchambuzi wa masuala ya kisiasa ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Jangwani, Baraka Mwaisabila amesema pamoja na kuwepo kwa idadi ndogo ya watu lakini mgombe huyo alipaswa kuwahutubia wale waliojitokeza pasipo kusubiri hadi namba ya watu iwe kubwa kama ilivyo kwenye mikutano ya vyama vingine vya siasa.


"Sisi tumeacha kazi zetu tumakuja kusikiliza sera za mgombea huyo lakini sasa kitendo cha kufika uwanjani na kuondoka bila kuhutubia na kuwaacha viongozi mkoa, wilaya na wagombea wa udiwani wakifanya hivyo peke yao si sahihi,” amesema Mwaisabila.

Naye, Vicent Kuligi ambaye ni katibu wa Muungano wa taasisi zisizo za kiserikali mjini Sumbawanga, alisema mgombea huyo wa urais kufika eneo husika na kutozungumza na wananchi aliowakuta anaonyesha jinsi chama chake kinavyotumia vibaya rasilimali zake.


“Huwezi kutumia rasilimali fedha haijalishi umepata ruzuku kutoka tume ya taifa ya uchaguzi au umetafuta kwa njia nyingine kufika pembezoni mwa nchi harafu hufanyi kampeni.....” amesema. 

Ameongeza kuwa kitendo cha namna hiyo kinafanya vyama hivi visiweze kuaminika katika jamii kwani haliingii akilini unatumia muda na fedha kufika kwenye mkutano halafu mgombea hataki kuhutubia.



Hata hivyo, haikubainika mara moja ni sababu zipi za msingi zilifanya mgombea huyo hasiutubie lakini kiongozi mmoja wa chama hicho wilaya alidai yeye si msemaji lakini mgombea wao hakuridhishwa idadi ya watu waliojitokeza.

Post a Comment

0 Comments