DC Nyamwese: Bilioni 1.3 kulipa fidia wananchi Mradi wa Gridi Imara Handeni
Handeni. Zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi waliopisha Mradi wa Gridi Imara limezinduliwa rasmi katika maeneo ya Mkata, Handeni na Kilindi, ambapo serikali imetenga Shilingi bilioni 1.3 kuhakikisha haki na maslahi ya wananchi yanalindwa.
Akizindua malipo hayo jana, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, alisema hatua hiyo ni kielelezo cha kuthamini mchango wa wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
> “Fidia hii ni kielelezo cha kujali utu na mchango wa kila mmoja. Tukiharibu au kutoheshimu miundombinu hii, hasara kubwa itakuwa yetu sote. Ni wajibu wetu kulinda mradi huu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Nyamwese.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Jafari Mpina, alisema serikali inalenga kuboresha mfumo wa umeme wilayani Handeni ili kuongeza upatikanaji wa nishati bora, hatua itakayochochea maendeleo ya kiuchumi kupitia biashara na ajira.
Naye, Meneja wa CRDB Tawi la Handeni, Carlos, alibainisha kuwa malipo yote ya fidia yataingizwa moja kwa moja kwenye akaunti binafsi za wanufaika, jambo litakaloongeza uwazi na usalama wa fedha.
Wananchi waliopokea fidia hiyo wameishukuru serikali, wakisema imewaongezea matumaini na kuwapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Bi Zainabu Mohamed, mkazi wa Mkata, alisema:
> “Kwetu sisi hii fidia ni faraja kubwa. Imetuwezesha kuanza upya maisha baada ya kupisha mradi. Tunashukuru sana kwa kuona mchango wetu umetambuliwa.”
Mzee Rashid Kinyau, mkulima wa Kilindi, naye alisema:
> “Kwa muda mrefu tulihofia kama kweli tutalipwa. Leo tumepokea fedha zetu na sasa tunaweza kuwekeza kwenye kilimo na elimu ya watoto wetu.”
Aidha, Neema Jumanne, kijana mkazi wa Handeni mjini, alibainisha kuwa fidia hiyo imewapa vijana nafasi ya kufikiria fursa mpya.
> “Kwa fedha hizi tutaanza miradi midogo ya biashara. Hii ni njia ya kushiriki moja kwa moja kwenye maendeleo ya taifa.”
Ends..
0 Comments