KISHINDO LA ALEX AKIZINDUA KAMPENI OLASITI ,AAHIDI OLASITI MPYA ITAWAKA TAA USIKU KAMA MCHANA,BARABARA ZA NDANI KUWA KAMA ULAYA , AELEZA MAFANIKIO LUKUKI KATIKA KIPINDI CHA MIAKA 10!

Na Joseph Ngilisho – Arusha


KAMPENI za Udiwani katika Kata ya Olasiti zimezinduliwa kwa kishindo, ambapo mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Alex Martin, ameahidi kuibadilisha sura ya kata hiyo kupitia barabara za lami, taa za barabarani, miradi ya maji, shule mpya na huduma bora za afya.

Uzinduzi huo umefanyika leo Septemba 26,2025 katika mkutano wa hadhara uliofurika wananchi, ukihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama, ambapo Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Arusha, Flora Zelothe, ndiye alikuwa mgeni rasmi na alimkabidhi Martin Ilani ya CCM, akimtaka akaisimamie na kuitekeleza ipasavyo.

>

“Tunamkabidhi ndugu yetu Alex Martin Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Wajibu wake sasa ni kuhakikisha wananchi wa Olasiti wananufaika na kila kipengele cha ilani hii. Wananchi muwe na imani naye, huyu ni kiongozi wa vitendo,” alisema Zelothe huku akishangiliwa na hadhira.


Katika mkutano huo, mgombea mwenzake wa CCM Kata ya Osunyai, Elirehema Nnko, alipanda jukwaani na kumnadi Martin kwa nguvu kubwa, akiwataka wananchi wa Olasiti kumpa kura za kishindo.

>

“Alex Martin ni diwani mchapakazi, ndiye chaguo sahihi kwa maendeleo ya Olasiti. Mkimchagua, mtakuwa mmechagua maendeleo ya kweli kwa vizazi vijavyo. Huu sio wakati wa kusikiliza maneno ya pembeni, huu ni wakati wa kumrudisha Alex ili aendeleze aliyoyaanzisha,” alisema Nnko.

Akihutubia wananchi, Martin alitaja mafanikio aliyoyasimamia ndani ya miaka 10 akiwa diwani, ikiwemo kufanikisha ujenzi wa barabara ya lami kutoka Talbani, na kuanzisha shule tatu za sekondari (Mrisho Gambo, Arusha Girls na Olasiti Sekondari).

>

“Olasiti ni moja ya kata chache nchini zenye shule tatu za sekondari. Hizi zote ni matunda ya jitihada zetu. Sasa tunajipanga kujenga shule mpya ya msingi kwa kuwa bado tunayo maeneo ya wazi,” alisema Martin huku akipigiwa makofi.



Aidha, aliahidi kuhakikisha barabara zote za ndani zinapitika kwa urahisi kwa kutumia katapila jipya lililonunuliwa na halmashauri, pamoja na kuendeleza miradi ya maji, afya na ulinzi.

>

“Wananchi wengi wanabambikiziwa ankara za maji bila kupata huduma. Kuna maeneo maji hayatoki kabisa. Hili lazima tulipiganie,” alisisitiza.


Kwa upande wa ulinzi, Martin alieleza kuwa maandalizi ya kuanzishwa kwa kituo cha polisi yamefikia hatua nzuri, kwani eneo na michoro tayari vimeshakamilika na suala hilo lipo ngazi ya IGP. Pia aliwahakikishia wananchi kuwa kituo cha afya kinachojengwa kitakamilika kwa muda mfupi.

Hata hivyo alisisitiza kuwa kilichopo mbele yake iwapo atachaguliwa ni kuhakikisha barabara ya kibo ambayo ipo katika mpango wa kuwekwa lami inakwenda kukamilika kwa wakati. 


Akizungumza jukwaani katika uzinduzi huo, Moses Severe, ambaye awali alimshinda Alex Martin kwenye kura za maoni kabla chama kurejesha jina la Martin, alionyesha mshikamano na mshindi huyo.


“Nimepanda hapa leo kuwaambia wananchi wa Olasiti kuwa sina kinyongo na ndugu yangu Alex. Mimi nipo tayari kushirikiana naye, kumpigia kura na kumtetea kwa nguvu zote. Namshukuru kila mjumbe aliyenipatia kura za ushindi, lakini pia nakishukuru chama chetu kwa maamuzi yaliyofanyika. Mimi nipo tayari kusubiri nafasi nyingine, Mungu akipenda,” alisema Severe akipigiwa makofi ya heshima.


Mmoja wa wananchi wa Olasiti, Neema John, alisema wanakiamini chama na mgombea wao kwa sababu ya kazi alizozifanya awali.

>

“Tunaona barabara zimeanza kubadilika, shule zimejengwa, na sasa tuna uhakika huduma za maji na afya zitaboreshwa. Kwa kweli Alex Martin anastahili kura zote za wananchi wa Olasiti,” alisema Bi. Neema kwa kujiamini.

“Olasiti Mpya Inakuja”

Akihitimisha uzinduzi huo wa kampeni, Alex Martin aliwaomba wananchi kumpa kura zote, akiahidi kushirikiana na viongozi wa mtaa na mabalozi wa nyumba kumi ili kukamilisha miradi yote kwa kasi kubwa.

>

“Olasiti tunayoipanga ni mpya – yenye barabara bora, taa zitakazowaka usiku, huduma za maji, shule nyingi, afya imara na ulinzi wa uhakika. Hapo ndipo tunapokwenda,” alisema kwa kujiamini huku akishangiliwa na wafuasi wa CCM.








Ends...

Post a Comment

0 Comments