KISHINDO CHA NASARI AKIZINDUA KAMPENI ARUMERU MASHARIKI HAIJAWAHI KUTOKEA,MAELFU WAFURIKA, MWIGULU ANOGESHA KAMPENI AMWOMBEA KURA ADAI WAMERU WAMELAMBA DUME

Na Joseph Ngilisho- ARUMERU


MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Joshua Nasari, amezindua kampeni zake kwa kishindo katika mkutano uliofurika maelfu ya wananchi na wafuasi wa chama hicho katika Kata ya Ngarananyuki, huku akiweka wazi dhamira yake ya kuibadilisha sura ya jimbo hilo kimaendeleo.


Katika uzinduzi huo  ulioshuhudiwa pia na Waziri wa Fedha na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Iramba, Mwigulu Nchemba, Nasari aliahidi kuanza mapinduzi ya maendeleo kwa kushughulikia changamoto kubwa za jimbo hilo, ikiwemo barabara na maji safi na salama.

Akihutubia maelfu ya wananchi kwa sauti ya msisitizo leo September 15,2025, Nasari alieleza kuwa uamuzi wake wa kuacha kazi ya ukuu wa wilaya aliyokuwa amepewa na Rais haukuwa rahisi, lakini aliona ni lazima arudi nyumbani kuwatumikia wananchi wake.

>

Nilikuwa nalindwa na askari wawili wenye silaha, nina gari la kiyoyozi na nyumba nzuri. Lakini niliamua kuacha hayo yote ili nije kuomba kazi ya wananchi—kazi yenye changamoto nyingi—kwa sababu najua Meru imesahaulika kwa muda mrefu,” alisema Nasari huku akishangiliwa.


>

Mama mkwe alinisihi nisiondoke serikalini, akisema ‘ukimkasirisha Rais utakosa kila kitu’. Lakini mimi nilikuwa na malengo ya kuwakomboa wananchi wangu, ndiyo maana nikaamua kuchukua maamuzi magumu.”


Nasari alisema jimbo la Arumeru Mashariki limekuwa likipigwa danadana kwa muda mrefu na limeachwa nyuma kimaendeleo. Aliahidi akipewa ridhaa ya wananchi, atasimama kidete bungeni kupigania ujenzi wa barabara za lami na mradi wa maji safi.

Alitaja barabara ya Ngarananyuki–King’ori na barabara ya Kikatiti–Sakila kuwa za kipaumbele, akisema ni muhimu kwa wananchi na wageni kutoka mataifa mbalimbali wanaokuja kuhubiri injili.

>

Meru imezungukwa na milima, lakini cha ajabu wananchi wake hawana maji safi na salama. Nikipewa ridhaa nitahakikisha changamoto hii inapewa kipaumbele serikalini,” alisisitiza.


Aidha, Nasari alimshukuru Mbunge anayemaliza muda wake, John Palangyo, kwa juhudi alizozifanya, lakini akasema bado changamoto kubwa zimebaki ambazo yeye ataendeleza mapambano bungeni.

Awali, akizungumza kabla ya kumkabidhi Nasari Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba aliwataka wananchi wa Arumeru Mashariki kujivunia kupata kiongozi huyo, akimwelezea kama kijana shupavu na mwenye uthubutu.

> Nasari si mtu wa maneno matupu. Hata alipokuwa katika chama kingine, mara kwa mara alikuwa anakuja kwangu na hata kwa Waziri Mkuu akipigania maendeleo ya Meru. Sasa mmeshapata kijana mzalendo na mpambanaji, wamelamba dume,” alisema Mwigulu.

Aidha, Nchemba alimtaka Nasari kusimamia ilani ya CCM mara atakapochaguliwa, na akamnadi Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya maendeleo iliyofanyika katika kipindi cha miaka minne pekee.

>

Rais Samia ameandika historia mpya katika sekta ya afya, elimu na miundombinu. Ameonyesha uaminifu mkubwa wa kusimamia fedha za umma, na miradi mikubwa iliyotekelezwa haiwezi kulinganishwa na awamu zilizopita,” aliongeza


Mwananchi mmoja mkazi wa Ngarananyuki, Theresia Kaaya, alisema wananchi wa Meru wameanza kupata matumaini mapya kupitia Nasari.

>

Kijana huyu anajua shida zetu, amezaliwa hapa na ameona tulivyoteseka bila maji na barabara. Tuna imani atatusaidia kweli kweli,” alisema huku akipigiwa makofi na wananchi wenzake.


Naye Mgombea Udiwani wa Kata ya Ngarananyuki kupitia CCM, Happy Saanya, alisema wananchi wa kata yake wako tayari kumpa Nasari kura za kishindo.

>

Ngarananyuki ni lango la maendeleo ya Meru, na Nasari ndiye kiongozi sahihi wa kulibeba jimbo hili mbele. Tutahakikisha tunampa kura zote,” alisema Saanya.

Kwa upande wake, mtia nia wa ubunge katika jimbo hilo, Profesa Daniel Palangyo, alimtaja Nasari kama kiongozi anayejitolea kwa dhati.

> “Nasari ameonyesha mfano wa kujitoa kwa maslahi ya wananchi. Maamuzi yake ya kuacha kazi serikalini kwa ajili ya kugombea ubunge ni ujasiri wa kipekee. Ni lazima tumpe ushirikiano,” alisema Prof. Palangyo.


Mkutano huo ulihudhuriwa na maelfu ya wananchi kutoka kata mbalimbali, ambao walimshangilia Nasari kila aliposisitiza kuwa hatakuwa mwoga kuieleza serikali changamoto za jimbo hilo.

Mwisho wa hotuba yake, Nasari aliomba kura za wananchi akiahidi kulibadili jimbo la Arumeru Mashariki na kulifanya kuwa kitovu cha maendeleo.











Ends....

Post a Comment

0 Comments