EALA YASIKILIZA KILIO CHA MADEREVA NA WAJASIRIAMALI NAMANGA
Na Joseph Ngilisho, LONGIDO
UMOJA wa Wabunge Wanawake wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) umeanza kushughulikia changamoto zinazowakabili madereva wa malori makubwa pamoja na wajasiriamali katika mpaka wa Namanga, unaounganisha Tanzania na Kenya mkoani Arusha.
Madereva waliokusanyika katika eneo la maegesho la Longido walisema mazingira ya eneo hilo si rafiki kutokana na kukosekana kwa huduma muhimu kama vyoo na maji safi, huku vumbi likihatarisha afya zao. Walisema sekta ya usafirishaji ni mhimili mkubwa wa uchumi wa Jumuiya, lakini huduma wanazopata haziakisi mchango wao.
Eliya Mnyuka, dereva mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 10, alisema:
"Kwa miezi kadhaa tumekuwa tukilazimika kuegesha malori kwenye eneo lisilo salama, bila maji wala choo. Wakati mwingine tunakaa siku tatu hadi wiki nzima tukijisaidia vichakani huku maofisa forodha wakitoa visingizio kama mtandao kufeli. Hata hivyo, tunatozwa shilingi 15,000 kwa maegesho duni yasiyo na huduma."
Madereva waliongeza kuwa ucheleweshaji wa vibali katika kituo cha forodha cha Namanga huwafanya wakae wiki nzima wakisubiri, jambo linalosababisha hasara kubwa kwao na kwa wafanyabiashara wanaotegemea usafirishaji huo. Wengine walisema paspoti za mwaka mzima hazitumiki ipasavyo upande wa Namanga, tofauti na mipaka mingine kama Mtukula, jambo linaloleta usumbufu usio wa lazima.
Joseph Mgovano, dereva kutoka Iringa, aliongeza kilio cha madereva akisema:
"Ni vyema magari yasiyo na mzigo yaruhusiwe kusafiri muda wote badala ya kuwekewa ukomo wa saa mbili pekee usiku. Aidha, ukaguzi wa namba za chasis unaofanywa na TRA unachukua zaidi ya saa tatu, jambo linalopoteza muda."
Mbali na madereva, wajasiriamali wadogo waliopo eneo la mpaka huo nao hawakubaki kimya. Sing’ati Paulo, muuzaji wa shanga na vito vya asili, alisema mtaji mdogo na soko dogo ni kikwazo kikubwa kinachowanyima kipato cha uhakika.
"Biashara zetu za shanga na virembo vya asili zinahitajika na wageni wanaopita, lakini changamoto ni mitaji midogo na kukosa soko kubwa. Pia maeneo tuliyopewa kufanya biashara hayana hadhi, ni duni mno, hakuna kivuli wala miundombinu ya kutuvutia wateja," alisema.
Naye Joyce Kabati, ambaye huuza shanga na mikufu ya kienyeji, aliongeza:
"Wajasiriamali wadogo wa mipakani tunahitaji kusaidiwa kupata mitaji nafuu na pia kupatiwa sehemu bora za kufanyia biashara. Hali ilivyo sasa hatupati nafasi ya kunufaika ipasavyo na wageni wengi wanaopita hapa Namanga."
Katika ziara hiyo, wabunge wa EALA waliambatana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Veronica Nduva, ambaye alisisitiza umuhimu wa kuboresha mazingira ya sekta ya usafirishaji na biashara ndogo ndogo.
"Forodha ya pamoja na soko la Jumuiya haviwezi kufanikiwa pasipo kuwepo kwa madereva wanaobeba bidhaa na wajasiriamali wadogo wanaochochea biashara mipakani. Ni wajibu wa serikali zote wanachama kuhakikisha vikwazo visivyo na tija vinaondolewa ili uchumi wa Jumuiya uendelee kukua," alisema Nduva.
Aidha, katika kuadhimisha Siku ya Wanawake, wabunge hao wa EALA pamoja na Katibu Mkuu walitumia ziara hiyo kusikiliza kero mahsusi za wanawake wajasiriamali wa Namanga na kuwatia moyo kuendeleza shughuli zao. Vilevile, walikabidhi msaada wa taulo za kike kwa wanafunzi wa kike wa shule zilizopo jirani na mpaka huo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukuza afya na elimu ya mtoto wa kike.
Kwa upande wake, Afisa Biashara wa Viwanda na Uwekezaji wa Halmashauri ya Longido, Ray James, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri, alieleza kuwa maegesho ya sasa ni ya dharura kwa kuwa maegesho rasmi ya Kimokoa yapo kwenye ukarabati.
"Baada ya ukarabati kukamilika, maegesho hayo yatakuwa na uwezo wa kuegesha zaidi ya malori 200 na yatahusisha huduma zote muhimu. Tunatarajia kukamilisha mwezi huu na kuanza kutumika ifikapo mwezi ujao, sambamba na mpango wa kupata shilingi bilioni moja kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya maboresho zaidi," alisema.
Ziara hiyo imetoa matumaini mapya kwa madereva, wajasiriamali wadogo na wanafunzi wa kike, huku wakiweka matarajio makubwa kwa viongozi wa Jumuiya kuhakikisha changamoto walizozitaja zinapatiwa majibu ya haraka ili kukuza biashara, elimu na uchumi wa kanda.
Ends.....
0 Comments