DKT NCHIMBI AZINDUA KAMPENI ZA CCM ARUSHA,AMNADI UBUNGE MAKONDA,GAMBO BADO HAONEKANI , ATAKA WATU KUTIKI OKTOBA MAGARI YA MAKONDA YAWA KIVUTIO

Na Joseph Ngilisho- ARUSHA 

MGOMBEA mwenza wa kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ameendelea na mikutano ya kampeni leo Ijumaa, Septemba 12, 2025, kwa kuhutubia mamia ya wananchi katika Uwanja wa Soweto jijini Arusha.


Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha, Dkt. Nchimbi alitumia fursa hiyo kuwanadi wagombea wa chama hicho akiwemo Mgombea Ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Ndugu Paul Christian Makonda, pamoja na wagombea wa nafasi za udiwani.


Aidha, Dkt. Nchimbi pia aliongoza uzinduzi rasmi wa kampeni za CCM kwa Jimbo la Arusha Mjini, akisisitiza kuwa chama hicho kimejipanga kuhakikisha linaendelea kuwatumikia wananchi kwa vitendo kupitia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025-2030.


“Ilani yetu inalenga kuinua maisha ya kila Mtanzania, kuimarisha huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika miaka mitano ijayo,” alisema Dkt. Nchimbi huku akipigiwa makofi na kelele za shangwe kutoka kwa wananchi.


Katika hotuba yake, mgombea mwenza huyo aliwataka wananchi wa Arusha na maeneo yote nchini kuhakikisha ifikapo Oktoba 29, 2025 wanajitokeza kwa wingi kupiga kura kwa mgombea urais wa CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na wabunge na madiwani wa chama hicho.


Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Paul Makonda, aliwahakikishia wananchi kuwa CCM imejipanga kushughulikia changamoto zinazowakabili hususan suala la ajira kwa vijana na kuboresha biashara ndogondogo.

“Tutahakikisha Arusha inakuwa kitovu cha fursa na maendeleo kwa wananchi wote bila kubagua,” alisema Makonda.


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Thomas Sabaya, alisisitiza mshikamo wa wananchi kwa wagombea wa chama hicho, akibainisha kuwa ushindi wa CCM ni chachu ya kuimarisha amani na umoja wa kitaifa.


Dkt. Nchimbi ambaye leo alianza rasmi mikutano ya kampeni katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, alianza na Longido, kisha Arumeru Magharibi na kukamilisha Arusha Mjini. Katika maeneo yote alikopitia, wananchi walimlaki kwa hamasa kubwa na kuahidi kuendelea kuiunga mkono CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao.








Ends..

Post a Comment

0 Comments