By Arushadigital – Tabora
KATIKA tukio linalotikisa siasa za mkoani Tabora, watu sita wamekamatwa na vyombo vya usalama kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa vinavyohusishwa na mchakato wa kura za maoni za ubunge jimbo la Nzega Mjini.
Wakati harakati hizo zikiendelea, mgombea mmoja wa ubunge aliyetajwa kuhusika kwenye sakata hilo ameripotiwa kutokomea usiku wa kuamkia Jumapili, akiiacha gari lake lenye kiasi kikubwa cha fedha – zaidi ya Shilingi milioni 16 – katikati ya mtaa wa Musoma, Nzega.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amethibitisha operesheni hiyo ya usiku ambayo imewaweka mtegoni watu hao, akisisitiza kuwa Mkoa wa Tabora hauna nafasi kwa siasa za kununua uongozi kwa fedha.
> “Hii siyo Tabora ya kununua uongozi. Tumewakamata watu sita waliokuwa wakihonga wajumbe. Mgombea anayehusishwa naye amekimbia na kuacha gari lake likiwa na pesa taslimu. Huu ni mchezo mchafu, na tutauvunja,” alisema kwa msisitizo.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani, mgombea huyo alionekana mara ya mwisho Jumamosi jioni akihudhuria mkutano na baadhi ya wafuasi wake, lakini baada ya fununu za kukamatwa kwa watu wake wa karibu, alichukua hatua za haraka kuondoka eneo hilo bila kuaga wala kutoa taarifa kwa chama chake.
Gari lake, lililokuwa na fedha na nyaraka mbalimbali, linashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Mkuu huyo wa mkoa amesema uchunguzi unaendelea na orodha ya watu zaidi ya 40 wanaodaiwa kuwa sehemu ya mtandao huo wa kuhonga imekabidhiwa kwa TAKUKURU kwa hatua stahiki. Aidha, amewataka wagombea wote wanaojihusisha na uchaguzi ndani ya vyama kuheshimu sheria na taratibu za uchaguzi bila kutumia fedha kama njia ya kushawishi wapiga kura.
> “Kwa sasa, usalama umeimarishwa. Kila mgombea aliyekuwa na nia ya kutumia ‘finishing’ ya fedha, ajue naye anatazamwa. Uongozi si biashara,” aliongeza Chacha.
Tukio hilo limeibua hisia kali kwa wakazi wa Nzega na wanachama wa chama tawala, ambapo baadhi yao wamepongeza hatua hiyo kama mfano wa kuigwa, huku wengine wakitoa wito kwa vyombo vya usalama kuongeza ulinzi na ufuatiliaji wa karibu katika maeneo mengine yenye uchaguzi wa ndani unaoendelea.
Ends...
0 Comments