POLISI WAPORWA MTUHUMIWA NA KUUAWA ,ALIUA MWENDESHA BODABODA KWA KUMTENGANISHA KICHWA,KICHWA KILICHOPOTEA CHAPATIKANA

By Arushadigital-Mwanza 


Jiji la Mwanza limepigwa na simanzi kufuatia tukio la kikatili la mauaji ya kijana dereva bodaboda, Dickson Yusuph (24), ambaye mwili wake ulipatikana bila kichwa katika mtaa wa Shadi, Kata ya Luchelele, kisha baadaye kichwa chake kupatikana msituni baada ya watuhumiwa wawili kuelekeza polisi eneo kilikofichwa.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Gideon Msuya, tukio hilo lilitokea Agosti 9, 2025, ambapo uchunguzi wa awali umebaini chanzo ni wivu wa mapenzi.

> “Marehemu alikuwa akihusishwa na uhusiano wa kimapenzi na mpenzi wa mmoja wa watuhumiwa. Walimvizia, kumshambulia kwa panga na kumtenganisha kichwa na mwili, kisha kuondoka na mali zake ikiwemo pikipiki na simu,” alisema Kamanda Msuya.


Watuhumiwa hao, waliotajwa kuwa ni Oscar Emmanuel (20) na Edwin Petrol (22), wote wakazi wa Shadi, walikamatwa katika msako wa haraka. Walikiri kuhusika na mauaji hayo na kuongoza polisi hadi msitu wa Nsumba walikoficha kichwa cha marehemu na baadhi ya mali zake.

Hata hivyo, wakati wa operesheni hiyo, kundi kubwa la wananchi wenye hasira kali walivamia eneo hilo na kushambulia watuhumiwa kwa silaha za jadi. Askari polisi walijaribu kuokoa hali lakini vurugu zilikuwa kubwa, na watuhumiwa wote wawili walipoteza maisha papo hapo. Askari wawili walijeruhiwa na kulazwa hospitalini.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Silivini, Ramadhan Malugu, alisema hasira za wananchi zilisababishwa na ukatili uliotumika kumuua marehemu.

> “Dickson alikuwa kijana mpole na anayeheshimika hapa. Watu walishindwa kuvumilia, wakaamua kuchukua sheria mkononi,” alisema.


Miili ya watuhumiwa imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa uchunguzi zaidi, huku mali za marehemu zikikabidhiwa kwa familia yake. Polisi wameonya wananchi kuepuka kujihusisha na vitendo vya kulipiza kisasi na badala yake kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake.

---

Post a Comment

0 Comments