MGOMBEA UDIWANI WA CCM ARUSHA,DOGO JANJA AMTWANGA RISASI MWANAFUNZI WA SEKONDARI

MGOMBEA UDIWANI CCM ADAIWA KUMPIGA RISASI MWANAFUNZI ARUSHA

Na Joseph Ngilisho- ARUSHA 


Arusha – Taharuki imetanda jijini Arusha baada ya Mgombea Udiwani wa CCM Kata ya Ngarenaro, Abdulaaziz Chende maarufu kama Dogo Janja, kudaiwa kumfyatulia risasi tatu mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Sombetini, Bakari Kharifa (17), akimtuhumu kuwa ni kibaka.


Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 4 usiku katika Mtaa wa Simanjiro, Kata ya Sombetini. Kwa sasa kijana huyo amelazwa hospitalini akipatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa vibaya miguuni kwa risasi.

Dada wa kijana huyo, Zaida Ramadhani, alisema alisikia milio ya risasi akiwa nyumbani.

“Nikiwa naangalia televisheni nilisikia risasi, nikamwambia mume wangu azime TV tusikilize. Baada ya muda nilihisi hofu maana wadogo zangu huwa wanapita nyumbani kwangu wakitoka kwa babu yao. Baadaye nilipigiwa simu kuambiwa mdogo wangu amepigwa risasi,” alisema.


Zaida alikanusha madai kuwa mdogo wake alikuwa kibaka au alimvamia Dogo Janja.

“Mdogo wangu siyo jambazi. Amejeruhiwa hovyo kwa risasi bila kosa lolote. Ni uongo kudai kuwa alikuwa anakaba ili kumpora,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa familia, mama mdogo wa Bakari alifika eneo la tukio na kumkuta Dogo Janja.

“Alimuuliza kwa nini amempiga risasi mtoto, lakini hakujibu kitu. Badala yake akaondoka kimya,” alieleza dada wa majeruhi.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, alisema tukio hilo lilitokea saa 5:30 usiku, ambapo inadaiwa kuwa wakati Abdulaziz Abubakari (30), mkazi wa Levolosi, alikuwa akishuka kwenye gari lake, alihisi kuvamiwa na Bakari aliyekuwa na mwenzake na kudai walikuwa na silaha ya jadi.


Katika kujilinda, Abdulaziz alitumia silaha aliyokuwa nayo na kumpiga risasi Bakari mguuni. Polisi wanasema watu wawili wanashikiliwa kuhusiana na tukio hilo huku uchunguzi zaidi ukiendelea.


Jeshi la Polisi limewahakikishia wananchi kuwa litatoa taarifa kamili baada ya uchunguzi kukamilika na kuwataka kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola ili kudhibiti matukio ya aina hiyo.


Hata hivyo, familia ya Bakari imeeleza masikitiko yao na kudai kuwa polisi wamekuwa wakikandamiza upande wao huku Dogo Janja akiendelea kuwa huru licha ya kumjeruhi kijana huyo kwa risasi.

“Kwa nini ndugu wanashikiliwa polisi wakati mtoto wetu amelazwa hospitali? Kwa nini Dogo Janja hajakamatwa wala kuhojiwa? Hii ni dhuluma. Mdogo wetu hana tabia ya wizi wala ukaba,” alisema Zaida kwa uchungu.


Wakazi wa maeneo ya Sombetini na Ngarenaro wameiomba serikali na vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina, wakisema tukio hilo limeibua hofu kubwa na kuacha maswali mengi kuhusu usalama wa wananchi dhidi ya matumizi ya silaha na mamlaka kwa wanasiasa ,wakisisitiza kuwa polisi inlinda kwa kuwa ni msanii mashuhuri na mgombea udiwani kupitia chama Tawala ccm.


Hata hivyo baadhi ya wakazi katika mtaa huo wa Simanjiro walidai kuwa mwanafunzi huyo alikuwa na wenzake wanne wakiwa na visu wakijaribu kumkaba dogo jaja ili kumpora ndipo alipo mfyatulia risasi kijana huyo na wenzake walifabikiwa kukimbia.


Ends..


Post a Comment

0 Comments