CCM ARUMERU MAGHARIBI YATUMA SALAAM,MSAFARA WA MGOMBEA UBUNGE KUCHUKUA FOMU WATIKISA,
MAMIA WAMSINDIKIZA DKT LUKUMAY .
Na Joseph Ngilisho- ARUMERU
MAMIA ya wanachama na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Arumeru Magharibi, leo Agosti 25, 2025, wamejitokeza kwa wingi kumsindikiza Dkt. Johannes Lukumay kuchukua fomu ya kugombea ubunge wa jimbo hilo, tukio lililotawaliwa na furaha, nderemo na vifijo.
Msafara huo ulioanzia eneo la Ngaramtoni ulihusisha magari ya matangazo, pikipiki na vikundi mbalimbali vya hamasa vilivyokuwa vimevalia sare maalum za chama, jambo lililoongeza shamrashamra za tukio hilo.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Dkt. Lukumay alisema hatua hiyo ni mwanzo wa safari ndefu ya mageuzi makubwa yatakayolenga kuleta maendeleo kwa wananchi wa Arumeru Magharibi, akisisitiza mshikamano na mshirikiano kama nguzo muhimu za kuimarisha demokrasia ndani ya chama na jamii.
"Namshukuru Mungu kwa hatua hii ya leo. Nina imani nitatekeleza ilani ya chama chetu kwa kushirikiana na wananchi wa jimbo hili. Nitaendelea kuinadi ilani ya CCM kwa vitendo na kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wa Arumeru Magharibi," alisema.
Aliongeza kuwa moja ya changamoto kubwa zinazolikabili jimbo hilo ni miundombinu ya barabara na kuahidi kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto hiyo pamoja na kuimarisha sekta nyingine za kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Mgombea udiwani wa Kata ya Mateves, Fred Ezekiel, alimshukuru Kamati Kuu ya Taifa ya CCM kwa kurejesha jina la Dkt. Lukumay na kuahidi kumpa ushirikiano wa karibu katika kuhakikisha jimbo hilo linabaki mikononi mwa CCM.
"Tunajivunia utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyofanywa na serikali katika maeneo mbalimbali ya jimbo hili. Ni wajibu wetu kushirikiana na wagombea wetu kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo endelevu," alisema Ezekiel.
Baada ya kukamilika kwa zoezi la kuchukua fomu, msafara huo uliendelea hadi nyumbani kwa Dkt. Lukumay, eneo la Ngaramtoni, ambako aliandaa chakula maalum kwa wafuasi wake kama sehemu ya shukrani kwa kujitokeza kumtia moyo.
Aidha, aliwashukuru wafuasi na wananchi kwa kumuunga mkono na kusisitiza kuwa mshikamano wao ndio utakaowezesha ushindi wa kishindo kwa CCM katika uchaguzi huo.
Mwisho
0 Comments