Na Joseph Ngilisho-Hai
KITUO cha Umahiri cha Kufua Umeme cha Kikuletwa,kilichopo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro kinatarajiwa kukamilika na kuanza kuzalisha umeme utakaounganishwa kwenye gridi ya Taifa ifikapo April ,2026 baada uingizaji wa mitambo muhimu ya kufua umeme kukamilika.
Kituo hicho,ni tawi la Chuo cha ufundi cha Arusha (ATC) na kinatekelezwa chini ya mpango wa Kikanda unaotekelezwa katika nchi za Afrika na Kusini (EASTRIP) kwa ufadhili wa benki ya dunia, kinatajwa kuwa miongoni mwa miradi ya kimkakati itakayosaidia kupunguza utegemezi wa wataalamu wa nje katika sekta ya umeme.
Akiongea na waandishi wa habari leo Agosti 4,2025,bà ada ya kutembelea mradi huo wenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 16.25 Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi stadi dkt. Fredrick Salukele alisema hatua ya awali ya ujenzi wa majengo imekamilika na kwamba ifikapo mwezi wa Oktoba,2025 kituo hicho kitaanza kupokea wanafunzi kwa ajili ya kujifunza ufuaji wa umeme.
"Hapa tunatarajia ifikapo oktoba mwanzo wa mwaka wa Masomo 2025 tutaanza kupokea wanafunzi ambao wanatarajia kusoma fani hizo zinazohusiana na ufuaji wa umeme.
Dkt Shekukele ambaye pia ni mratibu wa kitaifa wa EASTRIP,alisema kituo hicho kina malengo matatu , kufundisha, kijifunzia na kufanya tafiti na kwamba kukikamilika kitakuwa na manufaa ya kuongeza wataalamu wa ndani,Kuchochea Ajira na Ubunifu,Kuimarisha Ushirikiano wa Kikanda na Kuchangia Nishati Safi kwa Taifa.
Naye naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Baraza la vyuo vikuu la Afrika Mashariki,Frof,Idris Rai ambaye pia ni Mratibu Mradi wa EASTRIP,alisema wameridhishwa na maendeleo ya mradi huo ulipofikia, unaofadhiliwa na benki ya Dunia .
"Tumeridhishwa sana na maendeleo ya Mradi unaohusisha ujenzi wa majengo na kuhuisha ama kuimarisha nyenzo ya nguvu za umeme wa maji kilichojengwa na mjerumani 1930 na Sasa, kikiimarishwa na teknolojia ya kisasa"
Prof aliupongeza uongozi wa chuo cha ufundi Arusha kwa usimamizi mzuri wa mradi huo na kusema kuwa ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa Hidropower Megawati 1.6 zitakazounganishwa kwenye gridi ya taifa.
Mradi huu unafadhiliwa na benki ya dunia kupitia serikali ya Tanzania pia Kuna Kenya na Nchi ya Ethiopia ambao ni sehemu ya mradi na sisi baraza la vyuo vikuu tunasimamia huu mradi kwa nchi zote na tupo hapa kuangalia maendeleo ya mradi tumeridhika sana"
Kwa upande wake Mhandisi Emmanuel Norbert kutoka kampuni ya uhandisi inayotekeleza mradi huo ya HNAC Technology Campany LTD ya nchini China,alisema kwa sasa mradi huo umefikia asilimia 75 ya utekelezaji tangu kuanza mapema Mei mwaka jana 2024.
Alisema hadi kufikia desemba mwaka huu 2025,watakuwa wamekamikisha awamu ya kwanza wa utekelezaji wa mradi huo wa kufua umeme kutumia maji.
"Mradi huu upo katika awamu mbili na hatua ya kwanza ambayo tumeifikia kwa sasa ni hatua ya upauaji wa eneo la Pawer house na hatua inayofuata ni kuingiza mitambo ya ufuaji umeme tunayotarajia kuifanya wiki ijayo"
Naye Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha,Prof.Mussa Chacha alisema mradi huo ni maono ya serikali katika kuzalisha wanafunzi wenye ujuzi wa uhandisi wa umeme katika sekta ya nishati .
"Tunatarajia ifikapo Novemba mwaka huu 2025 tutapokea wanafunzi zaidi ya 600 watakao kuja kujifunza kozi mbalimbali za nishati jadidifu,ikiwemo uzalishaji wa umeme wa nguvu za jua, uzalishaji wa umeme nguvu ya upepo,uzalishaji wa umeme wa nguvu ya Maji "
Prof Chacha alisema kituo hiki kitakuwa na uwezo wa kutoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa fani ya umeme, wahandisi, mafundi sanifu na wataalam wa uzalishaji wa nishati jadidifu.
Kituo kitawezesha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa ndani na wa mataifa ya Afrika Mashariki. Kupitia teknolojia za hali ya juu, vijana watajifunza mbinu bora za uzalishaji wa umeme, hasa unaotokana na vyanzo safi kama maji, upepo na jua.
Ends....














0 Comments