CCM WASHTAKIWA MAHAKAMANI KWA KUMPITISHA SAMIA MGOMBEA PEKEE URAIS CCM


CCM Waitwa Mahakamani Kesi ya Uteuzi wa Samia Kugombea Urais

By Arushadigital -Dar es Salaam


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeitwa mahakamani kujibu kesi inayopinga uhalali wa uteuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.


Kesi hiyo imefunguliwa na Godfrey Malisa katika masjala kuu Dodoma Mahakama Kuu masijala  ndogo Dodoma ya Tanzania, inaelezwa kuwasilishwa na mwananchi mmoja ambaye anadai kuwa uteuzi wa Rais Samia haukufuata misingi ya katiba na taratibu za kisheria zinazoongoza uteuzi wa wagombea wa nafasi hiyo nyeti.


Katika hati ya madai, mlalamikaji anahoji mchakato wa uteuzi ndani ya CCM, akieleza kuwa ulikiuka baadhi ya kanuni na haki za kidemokrasia, na hivyo kuomba mahakama itangaze uteuzi huo kuwa batili. Aidha, mlalamikaji ameomba mahakama isimamishe mchakato wa kumpitisha mgombea huyo hadi kesi hiyo itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.


Mahakama tayari imeitaja kesi hiyo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu na imeagiza CCM kufika mahakamani kujibu madai hayo ndani ya muda wa kisheria uliowekwa. Kesi hiyo imevuta hisia za wanasiasa, wanaharakati na wachambuzi wa masuala ya kikatiba kutokana na unyeti wa nafasi ya urais na umuhimu wa mchakato wa kikatiba katika chaguzi.


Hadi sasa, viongozi wa CCM hawajatoa kauli rasmi kuhusu kesi hiyo, huku baadhi ya wachambuzi wakisema kesi hiyo inaweza kuwa na athari kubwa kisiasa endapo itapewa uzito na mahakama.


Kwa upande wake, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali bado haijatoa tamko rasmi kuhusu iwapo itajihusisha moja kwa moja katika shauri hilo kama mdau wa masuala ya kikatiba.


Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena wiki ijayo kwa ajili ya kupanga tarehe ya kusikilizwa rasmi, huku umma ukiendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa kesi hiyo ambayo huenda ikaweka historia mpya katika siasa za uchaguzi nchini.


Post a Comment

0 Comments