KESI YA TUNDU LISU YAPIGWA KALENDA TENA,LISU ASEMA. MASHAHIDI WANAPASWA KUONEKANA

By Arushadigital -DAR ES SALAAM

Upande wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutorusha mbashara mwenendo wa kesi hiyo wakati mashahidi wakiwasilisha ushahidi wao.


Maombi hayo yamewasilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali Nassoro Katuga mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Franko Kiswaga, wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo leo Agosti 13, 2025 kwa ajili ya kusikilizwa.


Wakili Katuga amesisitiza kuwa kesi hiyo ikiwa mbashara, mashahidi wanaweza kutambuliwa kwa ushahidi wao, jambo ambalo linaweza kuathiri uhuru wao katika kutoa ushahidi.


Kwa upande wake mshitakiwa Tundu Lissu ameendelea kusisitiza mahakama kutokubaliana na maombi hayo akidai kuwa mashahidi wanapaswa kuonekana ili umma uweze kujua namna kesi ya Uhaini inavyoendeshwa na haki iweze kutendeka kwa pande zote mbili.


Hata hivyo, Hakimu Kiswaga amesema hoja za upande wa Jamhuri na za utetezi zitatolewa uamuzi kulingana na taarifa muhimu kutoka Mahakama Kuu kuhusu kuwalinda mashahidi ambao ni raia.


"Leo hii nitaahirisha hadi tarehe ijayo kwa ajili ya kufanya commital procedure na sio tarehe tena kwa ajili ya maamuzi haya mawasilisho nitayatolea amri kwa tarehe hiyo kwa kuzingatia maamuzi ya Mahakama Kuu ambayo yalikuwa wazi yanahusu sio mashahidi wote bali yanahusu mashahidi ambao ni raia, hii taarifa ni kubwa kweli kweli kwahiyo lazima tujipe muda"Amesisitiza Hakimu Kiswaga


Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 18, 2025 kwa ajili maamuzi madogo kulingana na hoja zilizowasilishwa na pande zote mbili, na mshitakiwa amerejeshwa rumande.

Post a Comment

0 Comments