Na Joseph Ngilisho-Arusha
TAHARUKI ilitanda katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha baada ya ndugu ,jamaa na marafiki wa kijana aliyefariki dunia kuibua madai kwamba mwili wa marehemu ulizuiwa kutokana na malimbikizo ya bili ya hospitali yanayofikia kiasi cha sh, miluoni 910.
Tukio hilo lilitokea Jumatatu, Agosti 11, 2025, saa chache baada ya familia kufika hospitalini kuchukua mwili wa marehemu aliyepoteza maisha kutokana na ajali ya pikipiki iliyotokea usiku wa Agosti 9, 2025.
Maelezo ya Hospitali
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Kipapi Milambo, amekanusha vikali madai hayo, akisema taasisi yake inafuata mwongozo wa serikali wa kutozuia miili ya marehemu kutokana na madeni ya matibabu.
“Ni kweli kulikuwa na mawasiliano kati ya hospitali na ndugu wa marehemu kuhusu bili, lakini mwili haujawahi kuzuiwa. Kulikuwa na hali ya kutoelewana ambayo ilisababisha taharuki,” alisema Dk. Milambo.
Ameeleza kuwa gharama ya matibabu ya marehemu ilifikia takribani Sh 910,000, zikihusisha huduma za dharura, vipimo vya X-ray, CT-Scan na maabara vilivyofanyika kabla ya kifo chake.
Msimamo wa Familia
Kwa upande wao, ndugu wa marehemu wamesema walipokea taarifa ya deni kubwa lililowashangaza, wakidai halikuwa rahisi kulilipia kwa muda mfupi.
Albert Kilwembwi, Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilkiroa, Kata ya Lemara, alisema kuwa familia ililazimika kuomba msaada na kukopa ili kukusanya fedha, lakini bado hawakuweza kufikia kiwango kilichohitajika.
> “Tulikuwa tunahangaika kutafuta fedha. Tumeshirikisha waajiri na marafiki, lakini kiasi kilikuwa kikubwa mno,” alisema Kilwembwi.
Hali ya Taharuki
Mashuhuda walisema baadhi ya madereva bodaboda walijitokeza kuunga mkono familia, hali iliyosababisha mkusanyiko na mtafaruku nje ya chumba cha kuhifadhia maiti. Polisi waliwasili kudhibiti hali hiyo na kuhakikisha mwili unachukuliwa kwa taratibu.
Kauli Rasmi
Hospitali imesisitiza kuwa inaendelea kutoa huduma kwa kufuata miongozo ya serikali na kwamba familia yoyote inayokumbwa na changamoto ya kifedha inaweza kuomba mpango wa malipo bila kuzuia mwili wa marehemu.
ENDS...
0 Comments