DOCTA KAZOBA AWAVUTIA WATEMBELEAJI NANE NANE KWA KINYWAJI KIPYA CHA “KAZOBA NATURE ENERGY DRINK”
Na Joseph Ngilisho- Arushadigital
Arusha – Daktari maarufu wa tiba asili, Docta Kazoba, ameibua gumzo katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea jijini Arusha baada ya kutambulisha rasmi kinywaji kipya kinachojulikana kama Kazoba Nature Energy Drink.
Docta Kazoba, ambaye amejipatia umaarufu kwa mbinu zake za tiba asili na bidhaa za lishe, alitumia siku ya leo kutembelea mabanda mbalimbali, akibadilishana mawazo na kutoa elimu kwa wakulima, wajasiriamali na wataalamu wa sekta ya kilimo pamoja na watu mbalimbali walioshiriki naonesho hayo.
Akiwa amevalia vazi lake la kipekee la kitamaduni lililomfanya aonekane tofauti na kuvutia macho ya wengi, Docta Kazoba alitembea mabanda mbalimbali, akisalimiana na wakulima, wafugaji, wanafunzi na wageni wa maonesho huku akieleza historia ya kinywaji hicho kipya.
Akizungumza na wanahabari, Docta Kazoba alisema Kazoba Nature Energy Drink imetengenezwa kutokana na mimea ya asili, viungo vya tiba na virutubisho vinavyopatikana hapa nchini, lengo kuu likiwa ni kusaidia kuongeza nguvu za mwili, kuimarisha kinga na kumfanya mtu awe na uchangamfu muda wote.
Katika banda lake, mamia ya watembeleaji walijitokeza kuonja kinywaji hicho, huku wengine wakifurahia ladha yake na kununua kwa matumizi ya nyumbani. Baadhi waliita ni “kionjo kipya cha afya” kwenye soko la vinywaji vya kuongeza nguvu.
Maonesho ya Nane Nane mwaka huu yamekusanya zaidi ya washiriki 500 kutoka sekta za kilimo, ufugaji, teknolojia na bidhaa za viwandani, huku uvumbuzi wa Docta Kazoba ukionekana kuvutia umati na kuacha alama isiyofutika katika taswira ya maonesho hayo.
>
“Kazoba Energy Drink si kinywaji cha kawaida. Kinachanganya nguvu za asili na virutubisho muhimu vinavyosaidia mwili kuwa imara, kuongeza kinga na kumfanya mtu kuwa na uhai muda wote wa shughuli zake,” alisema Docta Kazoba huku akiwahimiza wananchi kutumia bidhaa za asili kwa afya bora.
Ends....
0 Comments