Marirta Kivunge aibuka mshindi wa kwanza viti maalum CCM Arusha
Na Joseph Ngilisho-ARUSHA .
MCHAKATO wa kupatikana kwa wagombea wa viti maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Arusha umefanyika kwa mafanikio ambapo Marirta Kivunge ameibuka mshindi wa kwanza kwa kupata kura 1,004 kati ya kura zote halali 1245 zilizopigwa, huku wabunge watetezi Catherine Magige na Zaytun Swai wakitupwa nje.
Nafasi ya pili ilishikwa na Chiku Issa, aliyepata kura 775, akifuatiwa na wagombea wengine waliokuwa wakiwania nafasi hiyo kwa ushindani mkubwa.
Uchaguzi huo ulifanyika Julai 30, 2025, katika ukumbi wa AICC jijini Arusha kwa usimamizi wa viongozi mbalimbali wa chama kutoka wilaya na Mkoa .
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi huo, Kenani Kihongosi Mkuu wa Mkoa wa Arusha alisema wapiga kura walikuwa 1261 kura zilizopigwa 1252, zilizoharibika 7, na kura halali ni 1245
Wengine walioshiriki mchakato huo ni pamoja na mbunge mtetezi wa nafasi hiyo Catherine Magige aliyeshika nafasi ya tatu kwa kuambulia kura 213,Asante Rabi Ngoyayi Lowate Kura 196,Zaytun Swai kura 141,Navsi Amo kura 50 na Lilian Bachi Kura 9.
Alisema jumla ya wagombea walikuwa nane wakiwania nafasi ya kuwakilisha wanawake kupitia viti maalum (UWT), lakini ni wawili hao waliopata kura nyingi zaidi na sasa watapelekwa katika hatua inayofuata ya mchujo ngazi ya taifa.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Marirta Kivunge aliwashukuru wajumbe wa mkutano kwa imani waliyoionesha kwake na kuahidi kuendeleza juhudi za kuwatetea wanawake na vijana katika sera za maendeleo.
>
“Ninashukuru kwa kura zenu, sitawaangusha. Nitakuwa sauti yenu na mtetezi wa maendeleo ya wanawake na jamii ya Arusha kwa ujumla,” alisema Kivunge huku akishangiliwa na wajumbe.
Kwa upande wake, Chiku Isla naye aliwashukuru wapiga kura wake na kusema kuwa ushindani huo umeonyesha ukomavu wa kisiasa ndani ya CCM na mshikamano wa wanawake katika kugombea nafasi za uongozi.
"Kipekee kuwashukuru wajumbe wote kwa kutimiza wajibu wenu ,mimi binafsi nasema asanteni niahidi kwamba mmenitwika mzigo mkubwaMmeniheshinisha mmenipa kura za heshma niwaahidi kwamba nitatumika pale nitakapohitajika"
Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha,Musa Matoroka katika hotuba yake, aliwapongeza wagombea wote kwa kampeni za amani na kuwataka washirikiane katika kuimarisha chama, bila kujali matokeo.
ends..
0 Comments