TWARIQA KUMUENZI SHEIKH DARWESHI KWA KISHINDO,YATANGAZA WIKI YA DARWESHI ,RAIS SAMIA ATAKIWA KUKAA MEZA MOJA NA WAPINZANI KUISAKA AMANI.

 Na Joseph Ngilisho- ARUSHA 


TAASISI ya Dini ya Kiislamu ya Twariqa- Zawiya Kuu Arusha ,Inatarajia kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha kiongozi wa taasisi hiyo Kongwe, Sheikh Salum Mubaraka Darweshi maarufu Darweshi 'Mti Mkavu' kwa kujitolea kuchangia  damu pamoja na kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kufanya usafi katika jiji la Arusha.

Darweshi ambaye alifariki Agosti 21 mwaka jana 2024 anatajwa kama kiongozi mwenye upendo kwa haki, mcheshi na kipenzi cha wengi katika jamii ya waislamu alipenda kufundisha dini,kujitolea kutunza mazingira ikiwemo kupanda miti.

Kwa mujibu wa Taasisi hiyo, maadhimisho hayo wataenda sanjare na  dua maalumu kwa ajili ya kuombea Taifa katika kipindi cha Uchaguzi.

Akiongea na vyombo vya habari leo Agosti 27,2025 makao Makuu ya Twariqa- Zawiya Kuu Arusha,Naibu katibu Mkuu Sheikh Haruna Husen alisema kuwa  maadhimisho hayo yanatarajiwa kuanza agosti  18 na kilele chake ni Agosti 21,2025.


"Kwa niaba ya Taasisi napenda kutoa taarifa kwamba tarehe 16 halmashauri kuu yenye wajumbe 13  itakutana hapa Zawiya Kuu ili kuandaa ratiba kamili ya maadhimisho ya wiki ya Sheikh Darweshi"


Alifafanua kuwa Agosti 18,2025 viongozi wote wa taasisi hiyo Tanzania wakiongozwa na Mkuu wa wilaya ya Arusha Joseph Mkude pamoja na timu yake  watachangia damu katika hospitali ya Rufaa ya Mt Meru.


Aliongeza kuwa "tarehe 19 mwezi wa 8, kabla ya Hauli, itakuwa kumbukumbu ya Kitaifa ambayo tutaiasisi hapa Zawiya Kuu Arusha ambayo itakuwa siku ya usafi na utunzaji wa mazingira katika kumuenzi marehemu Sheikh Darweshi"


"Katika tukio hilo tunatarajiwa kumwalika Mkuu wa Mkoa wa Arusha ,Kenani Kihongosi ili kushiriki katika jambo hilo ,ambapo  pia tutawaalika wageni mbalimbali"


Alisema Agosti 20 itakuwa ni usiku wa Sheikh Salum Mubaraka ,ambapo wanatarajia kufanya dua maalumu kwa ajili ya kuombea vijana waliolelewa na marehemu Sheikh Darweshi huku Kamishna wa uhifadhi Tanapa, Juma Kuji akipewa heshima ya kuwa mgeni rasmi wa mkesha wa tukio hilo.


Sheikh Haruna alisema kuwa Agosti 21, itakuwa ndio kilele cha maadhimisho hayo ambapo viongozi mbalimbali wa kitaifa watakaokuwa wamealikwa  watakuwepo.


Alisema Agosti 22  itakuwa ni siku  ya kuzulu kaburi la Marehemu sheikh Darweshi na siku inayofuata watahitinisha kwa dua maalumu ya kuombea vijana.


Katika hatua nyingine Sheikh Haruna aliwataka watanzania kuilinda amani ya Nchi kwa nguvu zote wakati Taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu.


"Sisi kama viongozi wa dini tunawajibu wa kuilinda amani tulioachiwa kama tunu ya Taifa na waasisi wa nchi hii"


Aliwaomba wanasiasa kuacha kauli zenye kuashiria uchochezi ambazo zinaweza kuleta  athari  kwenye kipindi cha uchaguzi.Alisisitiza kuwa maisha yapo hata baada ya uchaguzi hivyo siasa zisitutenganishe.


Sheikh haruna alimwomba rais samia Suluhu hasan kukaa meza moja na viongozi wa vyama vya siasa ili kudumisha amani na hivyo  kuondoa viashiria mbalimbali vinalenga kuharibu amani.


Naye sheikh Iddy Ngella alisisitiza suala la amani sio ombi bali kila mtu ni lazima kutoa kipaumbele katika kipindi chote cha uchaguzi.






Ends...



























Post a Comment

0 Comments