ARUSHA YAONGOZA KWA UKATILI WA KIJINSIA KWA WATU WAZIMA NA WATOTO – TAARIFA YA KUSHTUA

 ARUSHA YAONGOZA KWA UKATILI WA KIJINSIA KWA WATU WAZIMA NA WATOTO – TAARIFA YA KUSHTUA

By Arushadigital – Arusha

Mkoa wa Arusha umeibuka kuwa kinara wa matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watu wazima, huku pia ukiorodheshwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa ukatili dhidi ya watoto nchini, kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa na taasisi za ulinzi wa haki za binadamu.


Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Arusha imeongoza kwa idadi ya matukio ya unyanyasaji wa kingono kwa watu wazima, hasa wanaume, ukatili wa kisaikolojia, pamoja na matukio ya ubakaji na vitendo vya sodoma ambavyo vimeongezeka kwa kasi ya kutisha.


Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa mwaka 2023 imeonesha ongezeko kubwa la ukatili wa kijinsia kwa wanaume, ambao sasa wanaanza kujitokeza kuripoti visa vya manyanyaso, jambo ambalo awali lilikuwa nadra kutokea kutokana na mila na desturi za kukandamiza wanaume wanaonyanyaswa.


Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 10 ya matukio yote ya ukatili wa kijinsia kwa mwaka 2023 yalihusisha wanaume – ongezeko kutoka asilimia 4 mwaka uliotangulia. Wataalamu wa masuala ya kijamii wanasema hali hiyo inatokana na mabadiliko ya kijamii na ongezeko la uelewa kuhusu haki za binadamu.


“Katika maeneo mengi ya Arusha, tunashuhudia ongezeko la matukio ya wanaume kufanyiwa ukatili wa kimwili na kisaikolojia na wakati mwingine hata kingono. Hii ni ishara kwamba jamii inabadilika na sasa watu wanaanza kusema ukweli,” alisema Afisa wa Ustawi wa Jamii, Bi. Agnes Mollel.


Aidha, katika kundi la watoto, Arusha ilirekodi visa zaidi ya 1,000 vya ukatili ikiwemo vipigo, ubakaji, na kunyimwa haki za msingi kama elimu na matunzo. Hii inaifanya kuwa moja ya mikoa hatarishi zaidi kwa ustawi wa mtoto Tanzania.


Katika mkutano wa tathmini wa hali ya usalama wa kijamii uliofanyika jijini Arusha hivi karibuni, wadau walitoa wito kwa serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kuongeza juhudi katika kutoa elimu ya ulinzi wa haki za binadamu, hasa kwa makundi maalum kama wazee, wanawake, wanaume na watoto.


“Tunahitaji mabadiliko ya kimtazamo katika jamii. Ukatili dhidi ya mtu mzima – awe mwanaume au mwanamke – ni jambo linalopaswa kuchukuliwa kwa uzito sawa na ukatili dhidi ya watoto,” alisema Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Kanda ya Kaskazini, Bw. Elibariki Kimaro.


Pamoja na changamoto hizi, Arusha pia imepongezwa kwa kuwa mkoa ambao wananchi wake wanaanza kuamka na kuripoti matukio hayo kwa mamlaka husika, hatua inayosaidia katika upatikanaji wa takwimu sahihi na kuboresha mikakati ya ulinzi wa haki.


Mwisho


Post a Comment

0 Comments