TRA KAGERA YAJIVUNIA HUDUMA BORA YA WANANCHI

 TRA KAGERA YAJIVUNIA HUDUMA BORA YA WANANCHI


Na Lydia Lugakila  

Kagera

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera imeendelea kufanya vizuri katika upande wa makusanyo ya kodi huku ikijivunia huduma bora kwa wananchi, hasa wafanyabiashara walipa kodi wa mkoa huo.


Akizungumzia mafanikio hayo kupitia Maonyesho ya Saba Saba yanayoendelea katika viwanja vya CCM manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, Afisa Elimu na Mawasiliano wa TRA Kagera, Rwekaza Rwegoshora, amesema kuwa TRA imefanikiwa kutoa elimu ya kina kuhusu masuala ya kodi.


Amesema  Wafanyabiashara wamepata uelewa wa kutosha kuhusu jinsi ya kubadilisha umiliki wa magari, lakini pia TRA imetoa leseni za udereva, na kutoka Elimu ya  jinsi ya kutunza kumbukumbu za biashara zao pamoja na usajili wa biashara.


Rwegoshora ameongeza kuwa TRA Mkoa wa Kagera inaendelea kushirikiana na mikoa jirani, ikiwemo Geita, Mkoa wa kikodi Kahama, na Mara hasa katika eneo la Saba saba kwa lengo la kutoa huduma bora kwa Watanzania na wananchi wa Kagera ili wapate elimu mbalimbali kuhusu masuala ya kodi.


“Mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa sana hapa viwanja vya CCM  wameweza kupata elimu ya kutosha kama tunavyojua, misingi ya kodi ni miwili ambavyo mauzo pamoja na faida hivyo, kupitia elimu hii, mfanyabiashara atajua mauzo yake na faida yake, na matokeo, atalipa kodi iliyo sahihi na kulipa kiasi anachotakiwa kulipa kutokana na kutumia mashine za kielektroniki,” alisema Rwegoshora.


Amehimiza wananchi kutoa ushirikiano katika kuwafichua wale wote wanaojaribu kukwepa kulipa kodi, kufanya biashara bila kusajili, au kupita njia zisizo sahihi za uingizaji na uondoshaji wa bidhaa.


 Amewataka wafanyabiashara kushirikiana na mamlaka hiyo ili kutoa taarifa za wale wanaokiuka sheria za kodi, huku akisisitiza kuwa atakayetoa taarifa juu ya vitendo hivyo atapata zawadi kubwa ya asilimia 3 ya kodi itakayokusanywa.


Kuhusu makusanyo ya kodi, Rwegoshora ameongeza kuwa kwa TRA Mkoa wa Kagera, lengo lilikuwa ni kukusanya bilioni 164, lakini kufikia Juni 30, 2025, walikuwa wamekusanya shilingi bilioni 173, ambayo ni ufanisi wa asilimia 123.


Amesema kuwa  Mmafanikio hayo yamepatikana kutokana na utoaji wa elimu kupitia vyombo vya habari, ikiwemo redio, semina, na magari ya matangazo, pamoja na ushirikiano mkubwa wa viongozi wa serikali, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajjat Fatma Mwassa.


Hata hivyo, Rwegoshora amewakumbusha wale ambao hawakuweza kufanya makadirio ya kodi ya mwaka 2025 kufika katika ofisi za mamlaka hiyo kufanya makadirio yao mapema ili kuepuka riba na adhabu.

Post a Comment

0 Comments