TAASISI YA NELSON MANDELA YAADHIMISHA WIKI YA UBUNIFU

Na Joseph Ngilisho-ARUSHA


Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imeadhimisha Wiki ya Ubunifu kwa lengo la kuendeleza maono ya Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela, aliyetamani bara la Afrika lijitegemee kielimu na kiteknolojia kwa kuzalisha wataalamu wake wa ndani.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo Julai 16,2025 katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo, Makamu Mkuu wa Taasisi hiyo, Profesa Maulilio Kipanyula, alisema Wiki ya Ubunifu inalenga kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa sayansi, uhandisi, teknolojia na ubunifu kama nguzo kuu za maendeleo ya kweli.


“Maendeleo hayawezi kupatikana bila sayansi na teknolojia. Tumejikita pia katika matumizi ya sayansi shirikishi, hasa akili bandia (AI), kama sehemu ya kukuza maarifa ya vijana wetu,” alisema Prof. Kipanyula.


Shughuli hiyo imeambatana na mihadhara ya kitaalamu kutoka kwa wazungumzaji wa kitaifa na kimataifa, pamoja na maonesho ya bunifu kutoka kwa wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo vya ufundi. Kila kundi lilipewa nafasi kuonesha vipaji vyao kupitia uvumbuzi unaolenga kutatua changamoto za kijamii.




Miongoni mwa bunifu zilizovutia wengi ni drone iliyoundwa na wanafunzi wa shule ya sekondari ya St. Joseph, ambayo ina uwezo wa kupanda mbegu shambani kwa kutumia mfumo wa kisasa unaopima ukubwa wa shamba na kusambaza mbegu kwa usahihi na haraka.


“Nimefurahishwa sana na ubunifu huu. Teknolojia hii ni msaada mkubwa kwa wakulima wetu kwani inapunguza gharama, muda, na upotevu wa mbegu. Ni aina ya bunifu zinazofaa kuendelezwa,” aliongeza Prof. Kipanyula.


Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi anayeshughulika na Taaluma, Utafiti na Ubunifu, Prof. Anthony Mshandete, alisema taasisi hiyo inaendelea kuibua vipaji kuanzia shule za sekondari hadi vyuo vikuu kwa lengo la kukuza teknolojia zinazoibuka na kuliletea taifa maendeleo.


Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mandela Wiki, Prof. Linus Munishi, alisema wiki ya ubunifu imehusisha wadau kutoka ngazi mbalimbali kuanzia shule za sekondari, vyuo vya kati na vikuu, hadi mashirika ya umma, sekta binafsi, wajasiriamali na viwanda.


“Tunapenda kuona kizazi cha ubunifu kinaanza kuibuliwa mapema kabisa, ndiyo maana tumeshirikisha hata shule za awali na zile zilizoko karibu na taasisi,” alieleza Prof. Munishi.


Maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kukuza mawazo mapya na kushirikisha jamii katika safari ya mabadiliko ya kiteknolojia, kwa kuzingatia dira ya Hayati Nelson Mandela ya Afrika yenye kujitegemea kielimu na kisayansi.


Ends..

Post a Comment

0 Comments