MGOMBEA URAIS TANZANIA ABWAGA MANYANGA DAKIKA ZA JIOONI, ALIA KUTISHIWA MAISHA

Na Arushadigital-DODOMA

KUNJE NGOMBALE MWIRU ASITISHA KAMPENI ZAKE AKIDAI KUPATA VITISHO NA MATUSI

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), Kunje Ngombale Mwiru, ametangaza kusitisha kampeni zake za kisiasa akidai kuwa amekuwa akipokea simu za vitisho na matusi kutoka kwa watu wasiojulikana.

Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika mkoani Dodoma, Kunje alisema amechoshwa na mfululizo wa vitisho anavyovipata yeye na wasaidizi wake, hali iliyomfanya aamue kuacha kuendelea kunadi sera za chama chake hadi uchaguzi utakapofanyika.

> “Siasa imeletwa kwenye Taifa letu kwa sababu ya mabadiliko. Mabadiliko haya ni ya kidunia. Yaani wewe mtawala nikupongeze tu hata kama unafanya makosa? Hata mimi nikifika Ikulu, uchaguzi unaokuja nikosoeni, maana nitakuwa chama tawala. Unaponikosoa unanijenga. Kikubwa msinitukane — tusi ndio baya, lakini kukosoana kwenye majukwaa ni muhimu,” alisema Kunje kwa hisia kali.


Kunje alieleza kuwa vitisho hivyo vinatokana na watu wasiofurahishwa na sera zake za ukosoaji wa serikali iliyoko madarakani. Hata hivyo, alisema hatabadili msimamo wake kuhusu kueleza ukweli kwa wananchi kwa kuwa chama chake ni cha upinzani kinacholenga kuleta mabadiliko ya kweli.

> “Taifa linisikie, sitaendelea tena na mkutano wa aina yoyote ile. Naenda kulala. Kama kufa nitakufa mimi leo, kesho utakufa wewe. Hata ukinitisha mimi kwenye ukweli sitishiki. Nikisema kidogo tu tayari wanakasirika — sasa tusiseme?” alisema Kunje huku akionekana mwenye hasira.


Aidha, mwanasiasa huyo alisisitiza kuwa licha ya kusitisha kampeni, endapo atachaguliwa kuwa Rais, ataunda Baraza dogo la Mawaziri ili kupunguza gharama za serikali, na kuahidi kupambana vikali na rushwa, akidai ataweka utaratibu wa “kuwatumbukiza mafisadi kwenye bwawa la mamba” atakalojenga Ikulu.

Katika hatua nyingine, Kunje alionyesha kushangazwa na ongezeko la makongamano ya amani yanayoendelea kufanyika nchini, akisema hajui sababu ya mikutano hiyo kwani Tanzania ipo katika hali ya utulivu.

> “Ninashangaa kuona kila siku makongamano ya amani, na viongozi wa dini wako mstari wa mbele. Mimi sioni kama kuna vurugu nchini. Amani ipo, tusitumie jina la amani kujificha kwenye uoga wa kusema ukweli,” aliongeza.


Tangazo la Kunje limezua mjadala mpana miongoni mwa wafuasi wake na wachambuzi wa siasa, huku wengi wakitaka vyombo vya usalama kuchukua hatua za haraka kuchunguza vitisho hivyo vinavyodaiwa kutolewa dhidi yake.

Chanzo Masama-Media 


Post a Comment

0 Comments