MCHUNGAJI YAMKUTA AKAMATWA NA POLISI KWA TUHUMA ZA UCHOCHEZI MANYARA


Jeshi la Polisi mkoani Manyara limethibitisha kumshikilia Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Boay, wilayani Babati, Mchungaji Elieth Mtaita, kwa tuhuma za ushawishi mbaya.

Akizungumza leo kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani, amesema kuwa taarifa zilizokuwa zikisambaa zikidai kuwa mchungaji huyo ametekwa si za kweli, kwani kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.

“Ni kweli tunamshikilia mchungaji huyo kwa tuhuma za ushawishi mbaya. Hakutekwa na mtu yeyote kama inavyodaiwa mitandaoni; tunafanya uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo,” amesema Kamanda Makarani.

Hata hivyo, Kamanda huyo hakufafanua zaidi kuhusu aina ya ushawishi unaodaiwa kufanywa na mchungaji huyo, akisema kuwa taarifa kamili zitatolewa mara baada ya uchunguzi kukamilika.

Tukio hilo limezua taharuki miongoni mwa wakazi wa Boay, ambapo baadhi yao wameomba vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa haki na kuhakikisha ukweli unajulikana bila upendeleo.

Jeshi la Polisi Manyara limeendelea kuwasihi wananchi kuwa watulivu na kuacha kusambaza taarifa zisizo na uhakika mitandaoni, zikisema zinaweza kuathiri mwenendo wa uchunguzi unaoendelea.

Ends..





 

Post a Comment

0 Comments