Na Joseph Ngilisho- ARUSHA
MRADI ya maendeleo yenye thamani ya sh, bilioni 8.6 katika Jijini la Arusha inatarajiwa kuzinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru Julai 11,2025.
Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha Joseph Mkude amesema kati ya miradi hiyo ipo ya kijamii, ya wananchi, halmashauri na mingine ya Serikali Kuu ambayo yote itagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 8.6.
Aidha ameeleza kuwa miradi minne itatembelewa, miwili itawekewa mawe ya msingi na miwili kuzinduliwa ukiwemo mradi wa maji unaotekelezwa katika kata ya Moivaro unaotarajiwa kuhudumia wananchi takribani elfu kumi na moja wanaoishi wilaya za Arusha jiji na Arumeru.
Ametaja miradi mingine kuwa ni uzinduzi wa mashine ya kuchunguza Saratani ya Matiti iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni mia nne, mradi wa ujenzi jengo la utawala katika shule ya Terati iliyopo Kata Muriet na miradi mingine ya barabara za katikati ya Jiji zenye urefu wa kilomita 2.7.
Sambamba na miradi hiyo pia Mwenge wa uhuru utatembelea wafanyabiashara wadogo wa ufugaji nyuki.
"Miradi ipo mingi licha ya hii niliyoitaja kwa mfano mradi wa ujenzi wa stendi kubwa ya mabasi, soko la kilombero, ujenzi wa bustani katika kata ya Themi na miradi hii yote tayari wakandarasi wako katika maeneo ya utekelezaji kwa hatua za awali",
"Pia kuna mradi mkubwa wa ujenzi wa uwanja wa mpira wa AFCON unaendelea vizuri na unatekelezwa kwa fedha za Serikali Kuu, malengo ya serikali baada ya kukamilika kwa uwanja huo ni kuongeza pato la Taifa sambamba na kukuza uchumi wa kila mmoja" Amesema DC Mkude.
Ends .
0 Comments