MASKINI WANAFUNZI WA FAMILIA MOJA WAFA KWA AJALI KWENYE BODABODA WAKIENDA SHULE !

 By arushadigtal-MOROGORO


Wanafunzi wawili wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Morogoro pamoja na dereva wa bodaboda waliokuwa wakisafiri naye wamefariki dunia papo hapo baada ya pikipiki yao kugongana uso kwa uso na lori la mizigo eneo la Kihonda Bima, barabara kuu ya Morogoro–Dodoma.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amewataja marehemu hao kuwa ni Lusajo Mwang'onda, mkazi wa Mkomola, na Ghalbu Omary, mkazi wa Kihonda Maghorofani, ambao wote walikuwa wanafunzi wa kidato cha nne. Dereva wa bodaboda aliyepoteza maisha ametajwa kuwa ni Baraka Sajio, mkazi wa Kihonda Maghorofani.


Kwa mujibu wa Kamanda Mkama, ajali hiyo imetokea baada ya dereva wa bodaboda, ambaye pia ni miongoni mwa waliopoteza maisha, kujaribu kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari, na ndipo alipogongana uso kwa uso na lori lenye namba za usajili T 310 DQC lililokuwa likisafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma, likiwa na tela namba T 646 ANQ.


“Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa bodaboda aliyekuwa anataka kuyapita magari bila kuwa makini. Kwa bahati mbaya waligongana uso kwa uso na lori,” amesema Kamanda Mkama.

Miili ya marehemu wote watatu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.



Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Daniel Nkungu, amethibitisha kupokelewa kwa miili ya marehemu hao watatu.


“Leo asubuhi tumepokea miili mitatu wakiwemo wanafunzi wawili wa Shule ya Sekondari Morogoro na dereva wa bodaboda. Tayari miili hiyo imetambuliwa na ndugu wa marehemu na taratibu za mazishi zinaendelea,” amesema Dk. Nkungu.

Katika taarifa rasmi iliyotolewa na Uongozi wa Shule ya Sekondari Morogoro na kusambaa mitandaoni, uongozi umethibitisha vifo vya wanafunzi wao wawili waliokuwa wakielekea shuleni wakati wa ajali hiyo.


“Uongozi wa shule unasikitika kutangaza vifo vya wanafunzi wetu wawili vilivyotokea eneo la Kihonda Bima baada ya pikipiki waliyokuwa wamepanda kugongana na lori la mizigo wakiwa njiani kuelekea shuleni majira ya saa 1:00 asubuhi,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mwili wa mwanafunzi Ghalbu Omary unatarajiwa kuzikwa Ijumaa saa 10 jioni nyumbani kwao Kihonda Maghorofani, Morogoro.


Endss

Post a Comment

0 Comments