MKUTANO MAALUMU WA 59 WA BARAZA LA MAWAZIRI EAC WAANZA ARUSHA, KUANDAA NJIA YA MKUTANO WA WAKUU WA NCHI

 MKUTANO MAALUMU WA 59 WA BARAZA LA MAWAZIRI EAC WAANZA ARUSHA, KUANDAA NJIA YA MKUTANO WA WAKUU WA NCHI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA


Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha yameanza kuwa kitovu cha maamuzi mazito ya kikanda kufuatia kuanza kwa Mkutano Maalumu wa 59 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo, ukiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi Wanachama unaotarajiwa kufanyika Machi 7, 2026, jijini hapa.

Mkutano huo maalumu umeanza katika ngazi ya Wataalamu kuanzia Machi 2 hadi 3, 2026, ukiwa na jukumu la kupitia kwa kina agenda na taarifa mbalimbali zitakazowasilishwa katika ngazi ya Makatibu Wakuu Machi 4, kabla ya kuhitimishwa katika ngazi ya Mawaziri Machi 5, 2026.

Hatua hii ya maandalizi inaelezwa kuwa ni muhimu katika kuhakikisha maamuzi yatakayofikiwa na Wakuu wa Nchi yanakuwa yamepitiwa kwa umakini wa kitaalamu na kiutawala, sambamba na kuzingatia maslahi mapana ya wananchi wa ukanda wa Afrika Mashariki.


Ajenda Nzito za Maendeleo na Utekelezaji

Miongoni mwa masuala yenye uzito mkubwa yanayotarajiwa kujadiliwa ni kupokea na kuchambua Ripoti ya Mwaka ya Baraza la Mawaziri kwa kipindi cha Novemba 30, 2024 hadi Desemba 30, 2025, pamoja na ripoti ya utekelezaji wa maamuzi na maelekezo yaliyotolewa katika mikutano iliyopita ya Wakuu wa Nchi wa EAC.

Aidha, mkutano huo utashuhudia uzinduzi wa Mkakati wa Saba wa Maendeleo wa EAC (2026/27–2030/31), unaotarajiwa kuweka dira mpya ya ushirikiano wa kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Mkakati huo unalenga kuimarisha soko la pamoja, kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani, na kukuza biashara ya kikanda na kimataifa.

Katika hatua nyingine muhimu, Baraza litazindua rasmi Dhamana ya Forodha ya EAC (EAC Customs Bond/Guarantee), hatua inayotarajiwa kurahisisha usafirishaji wa mizigo katika mipaka ya nchi wanachama na kupunguza gharama za biashara, hivyo kuongeza kasi ya mtiririko wa bidhaa ndani ya Jumuiya.


Mageuzi ya Kisheria na Uongozi

Mbali na ajenda za kiuchumi, mkutano huo pia utajadili masuala ya kisheria na kiutawala, ikiwemo kuridhia na kusaini Miswada ya Sheria iliyopitishwa na Bunge la Afrika Mashariki, uteuzi wa Katibu Mkuu wa EAC, kuhuisha mikataba ya uteuzi wa Naibu Makatibu Wakuu, pamoja na uteuzi wa Majaji wa Mahakama ya Jumuiya.

Vilevile, washindi wa mashindano ya uandishi wa insha ya EAC watatambuliwa na kupewa zawadi, hatua inayolenga kuhamasisha ushiriki wa vijana katika masuala ya ushirikiano wa kikanda.

Tanzania Yashiriki Kikamilifu

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongozwa na Bw. Benjamin Mwesiga, Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Ujumbe huo unajumuisha wawakilishi kutoka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora; Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji; Wizara ya Fedha; Wizara ya Viwanda na Biashara; pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Ushiriki huo unaakisi dhamira ya Tanzania katika kuendeleza ajenda ya ujumuishaji wa kiuchumi na kuimarisha nafasi yake katika soko la kikanda.

EAC: Soko Kubwa, Fursa Pana

Kwa sasa, Jumuiya ya Afrika Mashariki ina nchi wanachama nane, ikiwa na idadi ya watu zaidi ya milioni 300 na pato la pamoja linalokadiriwa kuzidi dola za Marekani bilioni 300. Takwimu hizo zinaifanya EAC kuwa miongoni mwa jumuiya za kikanda zenye soko kubwa na fursa pana za uwekezaji barani Afrika.

Mkutano huu wa 59 wa Baraza la Mawaziri unatazamwa kama hatua muhimu ya kuimarisha mshikamano wa kisera na kiutendaji ndani ya EAC, huku macho na masikio ya ukanda yakielekezwa Arusha kusubiri maamuzi yatakayochochea mwelekeo mpya wa maendeleo ya pamoja.






Ends

Post a Comment

0 Comments