Na Joseph Ngilisho -ARUSHA
Watumishi 700 kutoka kwenye taasisi mbalimbali za serikali wanatarajiwa kushiriki katika mkutano wa kwanza wa Jumuiya ya Waalamu wa Usimamizi wa RasilimaliWatu na Utawala katika Utumishi wa Umma (TAPA-HR),utakaofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), 22 hadi 25 Julai,2025.
Hayo yalisemwa jana jijini Arusha na Mwenyekiti wa TAPA-HR, Grace Meshy,wakati akizungumza na waandishi wa habari na alisema mkutano utafunguliwa na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Utumishi wa Umma na Utawala Bora,George Simbachawene.
Alisema Jumuiya za Wataalamu hao,imeundwa kutekeleza malengo ikiwamo kuhakikisha kunakuwa na fursa ya kubadilishana uzoefu katika masuala ya usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala, kukuza ujuzi na weledi katika masuala ya usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala.
Pia alisema wanajukumu la kuhifadhi na kusambaza taarifa za kitaaluma katika kada ya usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala kwa njia ya machapisho, mikutano, ziara za mafunzo,makongamano ya kitaaluma, midahalo na kuweza kujiunga na mitandao ya kitaaluma ya kitaifa na kimataifa.
Mwenyekiti huyo,alisema malengo mengine ya kuundwa TAPA-HR ni pamoja na kuimarisha maadili ya kitaaluma katika masuala ya usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala,kukuza ushirikiano wa kitaifa na kimataifa kupitia mashirika na taasisi zinazojishughulisha na ukuaji na usimamiaji wa rasilimaliwatu na Kuimarisha utekelezaji wa mifumo inayotumika katika utumishi wa umma inayotumika katika usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala ili kufikisha huduma kwa umma na kuleta ustawi kwa umma.
Hata hivyo,alisema mkutano huo, umelenga kuwakutanisha wataalamu wa kada ya usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala katika Utumishi wa Umma kutoka Tanzania bara na visiwani ili kuwajengea uwezo zaidi na kuongeza tija katika ufikiaji wa malengo makuu ya taasisi zao na ustawi wa wananchi kwa jumla.
Alisema kamati ya maandalizi ya mkutano imeandaa mada mbalimbali zinazolenga kuimarisha utendaji kazi wa watumishi hao, na zitawasilishwa na wawezeshaji nguli katika utumishi wa umma ambao watapata nafasi ya kueleza uzoefu wao.
Aidha amewaomba waajiri wote katika Wizara,Tawala za Mikoa Mamlaka ya Serikali za Mitaa,Wakala wa Serikali,Mashirika ya Umma,Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki,pamoja na Idara zinazojitegemea kuwawezesha Wataalamu wao wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala kushiriki katika mkutano huo mkuu wa kitaalamu ili waweze kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao mahala pa kazi.
0 Comments