WAWILI WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA MATUMIZI MABAYA YA MITANDAO.
By Arushadigtal-ARUSHA
JESHI la Polisi Mkoani Arusha limetoa ufafanuzi kuhusiana na taarifa inayosambaa kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii ikieleza juu ya watu wawili kutekwa na watu wasiojulikana huko katika maeneo ya Maji ya Chai, wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha.
Akitoa ufafanuzi kuhusiana na tukio hilo leo juni 22,2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa na Jeshi la Polisi Juni 20 mwaka huu na kuwataja kuwa ni Jackson Kabalo (32) na Joseph Mrindoko (37) wote wakiwa ni wajasiriamali, wakazi wa Maji ya Chai wilayani Arumeru kwa tuhuma za matumizi mabaya ya mitandao.
Kamanda Masejo amebainisha kuwa upelelezi wa tukio hilo unaendelea na pindi utakapokamilika hatua zaidi za kisheria zitafuata.
Jeshi la Polisi Mkoani humo limetoa onyo kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii kuacha kusambaza taarifa ambazo hawana uhakika nazo zinazoleta taharuki katika jamii hasa zile za kuzusha kuwa watuhumiwa wamekamatwa na watu wasiojulikana jambo ambalo sio la kweli.
Ends..
0 Comments