EWURA YATOA NENO KWA MAWAKALA WA GESI KUHAKIKISHA WANAZINGATIA KANUNI ZA USALAMA NASHERIA ZABUOIMAJU WA UZITO WANAPOWAUZIA WATEJA.

 Na Joseph Ngilisho- ARUSHA 

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) – Kanda ya Kaskazini, imewataka mawakala wa gesi za majumbani (LPG) kuhakikisha wanazingatia kanuni za usalama na sheria za upimaji wa uzito kabla ya kuwauzia wateja mitungi ya gesi, ikiwemo kutumia mizani na kuhakikisha mitungi ina “seal”. 




Wale watakaobainika kukiuka taratibu hizo watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutozwa faini au kunyimwa leseni za biashara.




Akizungumza Alhamisi, tarehe 19 Juni 2025, wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wasambazaji na wauzaji wa LPG katika Jiji la Arusha, Meneja wa EWURA Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Lorivii Longidu alisema:

“Tumewakumbusha hatua tutakazozichukua tukiwakuta mawakala wa gesi hawana mizani za kupimia uzito wa mitungi kabla ya kuwauzia wateja. Kama mitungi haina seal, tutawapiga faini.”

 

Aidha, Mhandisi Longidu alieleza kuwa EWURA inaendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.




“Mkakati huu unalenga kuboresha afya za wananchi, kulinda mazingira na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ambao ni hatari kwa mazingira na afya,” alisema Longidu.
Meneja huyo pia alisisitiza wajibu wa watoa huduma kutoa elimu kwa wateja kuhusu usalama wa matumizi ya gesi:

“Wamesisitizwa kuelimisha wateja wao kabla ya kuwauzia mitungi ya gesi. Gesi isipotumika kwa usahihi inaweza kusababisha madhara makubwa.”



 

Mhandisi wa Petroli kutoka EWURA, Magreth Mwita, aliwaeleza washiriki utaratibu wa kupata leseni za kusambaza au kuuza LPG:

“Ni muhimu wafuate matakwa ya kisheria na ya kiufundi ili kuhakikisha usalama wa watumiaji na uendelevu wa biashara.”

 



Kwa upande wa sekta binafsi, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waagizaji na Wasambazaji wa LPG Tanzania, Mhandisi Amos Mwansumbule, alisema:

“Tunawahimiza mawakala ni lazima watumie mizani ili mteja ahakikishe mtungi wake kabla hajauchukua. Lengo letu ni kufikia asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ifikapo 2034.”

Akitaja changamoto kubwa, Mwansumbule alisema:

“Sasa kumetokea watu wanajaza mitungi ya gesi kiholela mitaani. Wanachukua mitungi ya wanachama wetu na kuijaza kwa ujazo mdogo, mtu ananunua mtungi wa kilo sita kumbe ni kilo tatu. Tunataka kushirikiana na EWURA kuwadhibiti.”

Aliongeza kuwa wasambazaji wa gesi wana wajibu wa kutoa elimu ya matumizi salama kwa kila ngazi ya usambazaji:

“Katika mnyororo wa usambazaji wa gesi tuna wadau wanne: msambazaji mkuu, msambazaji wa kati (distributor), wakala wa mtaani, hadi mtumiaji wa mwisho. Kila mmoja anawajibika kutoa elimu kwa anayemfuata.”



 

Nganashe Laizer, ambaye ni wakala wa kuuza gesi jijini Arusha, alisema semina hiyo imemsaidia kuongeza uelewa:

“Leo nimejua kuwa kumbe tunatakiwa tuwe na mizani na ile mitungi inapaswa kuwekwa eneo la wazi lenye hewa ya kutosha, pamoja na kuonyesha bei elekezi.”

Hata hivyo, Laizer alilalamikia ushindani usio wa haki kutoka kwa wafanyabiashara wasiokidhi vigezo:

“Changamoto ni kwamba kuna watu wameingia kwenye biashara ya gesi bila vigezo. Mtu ana duka dogo tu, anaweka mitungi, wengine wanauza bei ya chini kuliko elekezi. Sisi tumewekeza fedha nyingi lakini tunaharibiwa.”

Alisema hali hiyo itapatiwa suluhu iwapo mamlaka zitasimamia utekelezaji wa sheria:

“Iwapo kila mmoja atazingatia sheria, vigezo, na kuweka mitungi sehemu salama na kwa bei elekezi, tutafanya biashara kwa haki.”

EWURA imeahidi kuendelea na kampeni za elimu kwa umma, ukaguzi wa mara kwa mara, na kuwachukulia hatua wafanyabiashara watakaoshindwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa ili kulinda usalama wa wananchi na mazingira.

Ends...



Post a Comment

0 Comments