FRIENDS OF BATULI YASAIDIA WATOTO WENYE CHANGAMOTO YA AKILI NA USONJI, UKIWAONA LAZIMA.MACHOZI YAKUTOKE,MKURUGENZI WA KITUO APONGEZA AITA WENGINE KUSAIDIA!

 Na Joseph Ngilisho ARUSHA 


KIKUNDI cha Kijamii cha Friends of Batuli cha jijini Arusha,kimetoa msaada wa kujikimu wa vitu mbalimbali ikiwemo vyakula  kwa watoto wenye changamoto ya ulemavu wa akili na usonji wanalolelewa na taasisi ya Mountain of Joy Foundation iliyopo Muriet ,Bondeni Jijini hapa.

Msaada huo ambao umekabidhiwa na kiongozi wa kikundi hicho Mwl.Batuli Kisaya ni pamoja na Mabati, Mahindi,Mchele ,Mikate na Dagaa ikiwa ni michango ya wadau wa  kikundi hicho Maalumu kwa kusaidia jamii yenye uhitaji.

Akiongea mara baada ya kukabidhi msaada huo,Mwl Kisaya alisema kuwa wao kama kundi la kijanii wameguswa na hali za watoto hao wanaolelewa na taasisi hiyo baada ya kutembelea na kujionea hali zao na kubaini uhitaji, ndipo alipokutana  na kuamua kujitoa kwa msaada huo uliowashirikisha pia wadau wa maendeleo.

Alisema siku ya kwanza kufika katika kituo hicho alilazimika kumwaga machozi baada ya kujionea changamoto cha  hao wenye ulemavu wa akili ambao malezi yao ni kazi kubwa.

"Nilifika katika kituo hiki na baada ya kujionea na kupewa maelezo ya maisha yao  kwakweli nililia machozi sio kazi rahisi kuishi na watoto wenye shida hii,nikazi kubwa,ndio maana tuliamua kujichanga na kusaidia kwa kile tulichojaliwa"Alisema.

Mmoja ya wanakikundi Glory  Kaaya alisema kilichowasukuma kujichanga na kuja kutoa msaada huo ni uchungu walioupata baada ya kujionea changamoto za watoto hao.

"Kilichotusukuma kuja kusaidia hapa sio kwamba sisi ni matajiri sana ila ni uchungu wa watoto hawa kutokuwa nacho kabisa na kuamua kusaidia jamii kwa kile tulichobarikiwa"Alisema.

Alisema kilichowasikitisha ni namna ya kuendesha maisha ya watoto ambao wengi wao hawajitambui,pia waliambiwa kituo hicho hakina mfadhili bali kinategemea michango ya wahisani.
Awali Mkurugezi wa taasisi ya Mountain of Joy Foundation,Elia Dyitege alisema kuwa taasisi hiyo inajihusisha na utoaji wa elimu na ujuzi kwa watoto wenye changamoto ya akili na usonji na wamekuwa wakichukua watoto kuanzia miaka 10 mpaka 22.

Alisema hadi sasa wanajumla ya watoto wapatao 31 ambao wanawapatia elimu ya ujuzi ili kuwasaidia kuweza kujimudu kuendesha maisha yao.

Alisema changamoto kubwa kwa watoto wa aina hiyo ni pamoja na uharibifu wa vitu,ugomvi pamoja na ukosefu uzio ambao unasababisha watoto kutoroka na kufanya  uharibifu mitaani.

Alisema taasisi hiyo kwa sasa haina mfadhili bali wanategemea wadau wa ndani kwa ajili ya kuendesha kituo hicho na sasa wanauhitaji wa vyakula,fedha kwa ajili ya ulipaji wa Kodi ya majengo ambayo wamepanga,Bili za Maji umeme pamoja na nguo kwa ajili ya watoto hao.

Mkurugenzi huyo aliwaomba wadau wa maendeleo kujitokeza zaidi na kuwasaidia ili waweze kumudu kuendesha taasisi hiyo .








Ends...



Post a Comment

0 Comments