MSUMI AHAIDI USHIRIKIANO KWA DC LUGANGIRA
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha (Arusha DC), Seleman Msumi, ameahidi kumpa ushirikiano Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kutatua kero za wananchi na kuimarisha uwajibikaji katika utumishi wa umma.
Msumi alitoa ahadi hiyo katika hafla ya Lugangira kukabidhiwa rasmi ofisi, akisema yeye pamoja na timu ya menejimenti ya halmashauri hiyo wako tayari kutekeleza maelekezo yatakayotolewa na Mkuu huyo wa Wilaya kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya wananchi wa Arumeru.
Alisema ushirikiano kati ya viongozi wa wilaya na halmashauri ni msingi muhimu wa kufanikisha majukumu ya Serikali, akiahidi kuendelea kushirikiana na Lugangira katika kusimamia shughuli za maendeleo.
“Mheshimiwa DC, kutoka ndani ya moyo wangu, tunakuahidi ushirikiano. Mimi pamoja na timu ninayoiongoza, wakuu wa idara, vitengo na watumishi wengine, tutapokea na kutekeleza maelekezo yote uliyoyatoa,” alisema Msumi.
Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Lugangira, akisema katika muda mfupi tangu kuanza kwa majukumu yake ameonesha kuwa na maono makubwa ya kuendeleza Arumeru.
Msumi alisema halmashauri itaendelea kuimarisha usimamizi wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kudhibiti mianya ya ubadhirifu na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Alisema pia kuna utaratibu wa kliniki za kusikiliza na kutatua kero za wananchi kila Ijumaa katika ngazi za kata na vijiji, akiahidi kuendeleza juhudi hizo kwa kushirikiana na Mkuu huyo wa Wilaya.
Katika hatua nyingine, Msumi alieleza kuwa Arusha DC ina fursa kubwa za kukuza utalii, akitaja maporomoko ya maji ya Napulu, maeneo yenye vivutio vya ikolojia na matukio ya michezo yanayovutia washiriki kutoka mataifa mbalimbali.
Alisema hivi karibuni wilaya hiyo iliandaa mashindano ya marathoni yaliyoshirikisha washiriki kutoka zaidi ya nchi nane, hatua inayochangia kuitangaza Arumeru na kufungua fursa za kiuchumi.
Alisisitiza kuwa kwa ushirikiano wa viongozi na watumishi wa Serikali, maono ya kuifanya Arumeru kuwa eneo lenye mvuto wa kimataifa yanaweza kutekelezwa na kuleta manufaa kwa wananchi.
Ends


إرسال تعليق