WANANCHI 3,500 WAPATA HUDUMA ZA MACHO BILA MALIPO KOROGWE

WANANCHI 3,500 WAPATA HUDUMA ZA MACHO BILA MALIPO KOROGWE

Na Hadija Bagasha, Korogwe

WANANCHI zaidi ya 3,500 wamejitokeza kupata huduma za uchunguzi, matibabu, dawa, miwani na upasuaji wa macho bila malipo katika Kambi ya Matibabu ya Macho iliyofanyika Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Mkoa wa Tanga.

Kambi hiyo ya siku tatu iliandaliwa na LALJI FOUNDATION na BARAKA FOUNDATION kwa kushirikiana na VISION 4 ALL EYE CENTER, ikiwa na lengo la kuwafikishia wananchi huduma za afya ya macho bila gharama.




Mwenyekiti wa LALJI FOUNDATION, Imtiaz Lalji, amesema jumla ya wagonjwa 333 walifanyiwa upasuaji wa macho katika kipindi cha kambi hiyo, huku 291 wakibainika kuwa na tatizo la mtoto wa jicho (cataract).

Amesema wagonjwa wengine 39 walibainika kuwa na matatizo mbalimbali ya macho yaliyohitaji huduma za upasuaji.

Mbali na upasuaji, Lalji amesema wananchi 1,723 walipatiwa dawa kulingana na mahitaji yao ya kiafya, huku wengine 1,706 wakipewa miwani ya kusomea.

Amesema mwitikio mkubwa wa wananchi katika kambi hiyo unaashiria kuwepo kwa changamoto kubwa ya magonjwa ya macho katika jamii, pamoja na changamoto ya baadhi ya wananchi kupata huduma kwa wakati kutokana na gharama na umbali wa vituo vya huduma.

“Takwimu zilizopatikana katika kambi hiyo zinaonesha ukubwa wa changamoto ya magonjwa ya macho katika jamii,” amesema Lalji.

Amesema wananchi wa maeneo ya vijijini ni miongoni mwa makundi yanayokabiliwa zaidi na changamoto ya kupata huduma za macho kwa wakati, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kupeleka huduma hizo karibu na wananchi.

Lalji amesema taasisi yake itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kuwafikia wananchi wenye uhitaji, hususan katika maeneo ambayo huduma za afya ya macho hazipatikani kwa urahisi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Zahara Msangi, amesema kambi hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi kwa kuwa imewawezesha kupata uchunguzi, dawa, miwani na huduma za upasuaji bila gharama.

Ameishukuru LALJI FOUNDATION, BARAKA FOUNDATION na VISION 4 ALL EYE CENTER kwa kushirikiana na Serikali kufikisha huduma hizo kwa wananchi wa Korogwe na maeneo jirani.

Msangi amewataka wadau wengine kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu karibu na maeneo wanayoishi.

Naye Mratibu wa Huduma za Macho Mkoa wa Tanga, Dkt. Husein Abassy, amesema ujio wa huduma hizo umesaidia kuwafikia wananchi wenye changamoto za macho ambao, kwa sababu mbalimbali, wanaweza kuchelewa kufika katika vituo vya afya.

Amesema utoaji wa huduma za uchunguzi na matibabu kwa wananchi katika maeneo yao ni muhimu katika kuwabaini mapema wenye matatizo ya macho na kuwapa matibabu stahiki kabla hali zao hazijawa mbaya zaidi.

Baadhi ya wananchi walionufaika na kambi hiyo wameeleza kuwa huduma walizopata zimekuwa msaada mkubwa kwao, hasa kutokana na ukweli kwamba baadhi yao wasingeweza kumudu gharama za matibabu na upasuaji wa macho.

Wameziomba taasisi, mashirika na wadau wengine kuendelea kushirikiana na Serikali kuandaa kambi kama hizo mara kwa mara ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini.

Kambi hiyo imekuja wakati ambapo changamoto ya magonjwa ya macho ikiendelea kuwa miongoni mwa masuala yanayohitaji kupewa kipaumbele katika jamii, huku mwitikio wa wananchi Korogwe ukisisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za uchunguzi, kinga na matibabu ya macho.

Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم