Breaking🔥

SAMIA AWACHANA MA-RC: “VITAMBI VITOKE” — AMSHUKIA MNYETI GEITA: “USIENDE KUJITAJIRISHA”AMTAKA AACHANE NA VIJIWE

SAMIA AWACHANA MA-RC: “VITAMBI VITOKE” — AMSHUKIA MNYETI GEITA: “USIENDE KUJITAJIRISHA”AMTAKA AACHANE NA VIJIWE 

Na Joseph Ngilisho | ZANZIBAR

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka Wakuu wa Mikoa nchini kuachana na maisha ya starehe na badala yake kujikita katika kuwatumikia wananchi, akisisitiza kuwa viongozi hao wamepewa dhamana ya kusimamia maendeleo na kutatua changamoto za wananchi.

Rais Samia alitoa kauli hiyo jana wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali, wakiwemo Wakuu wa Mikoa, katika hafla iliyofanyika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, ambapo alitoa maelekezo mazito kuhusu namna viongozi hao wanavyopaswa kutekeleza majukumu yao.

Akizungumza kwa msisitizo, Rais Samia alisema Wakuu wa Mikoa hawajateuliwa kwenda kwenye maeneo yao kwa ajili ya starehe, bali wamepewa dhamana ya Serikali inayowataka wafanye kazi kwa bidii na kusimamia maslahi ya wananchi.

“Hatuwapeleki pale mkale raha. Mkaichape kazi kweli kweli kuwatumikia wananchi. Sasa hayo matumbo yatoke kwenye mikoa,” alisema Rais Samia.

Alisema kila changamoto inayotokea katika mkoa ambao Mkuu wa Mkoa anauongoza ni sehemu ya dhamana yake na kwamba kiongozi huyo hapaswi kusubiri kila jambo lifanyiwe kazi na Serikali Kuu.

“Mkoa hauna fedha ni lako. Mkoa una matatizo ni lako. Umekumbwa na mazingira ambayo yamenyesha sana ni lako. Kila jambo linalotokea pale ni lako. Kwa Rais ni msaada tu,” alisema.

Rais Samia aliwataka Wakuu wa Mikoa kujiona kuwa ndiyo viongozi wakuu wa maeneo yao na kuchukua jukumu la kuhakikisha Serikali inafanya kazi kwa ufanisi na wananchi wanapata huduma na maendeleo.

“Jichukulieni kama ndiyo Rais wa eneo lile. Unabeba dhamana ya mkoa, unasema mkoa na watu wake hawa ndiyo taifa langu,” alisema.

Alisisitiza kuwa nafasi ya Mkuu wa Mkoa si ya kuwa “mfalme” wa eneo, bali ni ya utumishi wa wananchi na usimamizi wa shughuli za Serikali.

MNYETI APEWA ONYO

Katika hotuba hiyo, Rais Samia alimpa Mkuu wa Mkoa mpya wa Geita, Alexander Mnyeti, maelekezo maalumu, akimtaka kwenda katika mkoa huo kusimamia shughuli za kiuchumi na rasilimali kwa maslahi ya wananchi na Serikali badala ya kutumia nafasi hiyo kujitajirisha.

Geita ni miongoni mwa mikoa yenye shughuli kubwa za madini nchini, hali inayoufanya mkoa huo kuwa na umuhimu mkubwa katika ukusanyaji wa mapato na uchumi wa Taifa.

Rais Samia alisema Serikali imeweka mazingira yanayowawezesha wachimbaji wadogo na wafanyabiashara kufanya shughuli zao, hivyo jukumu la Mkuu wa Mkoa ni kuhakikisha shughuli hizo zinasimamiwa ipasavyo na Serikali inapata kodi stahiki.

“Sijakupeleka ukajitajirishe, nimekupeleka ukasimamie wanautajirika, walipe kodi zetu, waendelee kufanya kazi zao na mkoa upate maendeleo,” alisema.

Kauli hiyo ilikuwa ujumbe wa moja kwa moja kwa Mnyeti kuhakikisha utajiri unaopatikana Geita unaleta manufaa kwa wananchi na Taifa, huku wanaofanya shughuli za kiuchumi wakitimiza wajibu wao wa kulipa kodi.

“ACHANA NA VIJIWE VYAKO”

Rais Samia pia alimwonya Mnyeti dhidi ya kuruhusu mahusiano yake ya zamani na makundi ya watu aliokuwa akishirikiana nayo katika maeneo aliyowahi kufanya kazi kuathiri utekelezaji wa majukumu yake mapya.

Mnyeti amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi, ikiwemo kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mbunge na Naibu Waziri, kabla ya kupewa jukumu la kuongoza Mkoa wa Geita.

Rais Samia alisema anapaswa kwenda Geita akiwa na mtazamo mpya wa kiutendaji na kutenganisha urafiki na majukumu ya Serikali.

“Vile vijiwe vyako ulivyokuwa navyo huko nyuma nataka uwachane navyo. Usiache marafiki, lakini usiwa-entertain kwenye kazi yako,” alisema.

Alimtaka Mnyeti kusimamia kwa uadilifu shughuli za madini na kuhakikisha wanaonufaika na rasilimali hizo wanatimiza wajibu wao kwa Serikali na wananchi.

“Kwa hiyo nenda kasimamie vema. Jamaa zetu watakuwa nyuma yako wakikuangalia kwa karibu zaidi,” alionya.

“VITAMBI VITOKE”

Kauli ya Rais Samia kuhusu “vitambi” imekuwa msisitizo wa viongozi kuachana na starehe na kutumia muda wao mwingi katika kutatua changamoto za wananchi.

Alisema dhamana waliyopewa Wakuu wa Mikoa inawataka kuwa mstari wa mbele katika kusimamia utekelezaji wa sera na miradi ya Serikali, huku wakihakikisha wananchi wanapata huduma stahiki.

Rais Samia alisema ujumbe huo unawahusu viongozi wa Serikali kwa ujumla katika pande zote za Muungano, akiwataka kufanya kazi kwa kujituma na kuhakikisha kipindi chao cha uongozi kinaacha alama ya maendeleo.

“Mkaichape kazi kweli kweli kuwatumikia wananchi. Matatizo ya mkoa ule ni ya kwenu,” alisisitiza Rais Samia.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم