MALISA ASIMULIA ‘USIKU WA MATESO’ NAMANGA HADI ARUSHA
....Alivyokwama Nairobi, akavuka kwa gari, akakamatwa Namanga na kupelekwa kituo cha Diplomasia na Utalii
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Malisa, ambaye alikuwa akirejea nchini baada ya kukaa Marekani kwa zaidi ya miezi tisa, amesema hakutarajia kwamba safari yake ya kurejea nyumbani ingemalizika kwa kushikiliwa usiku kucha katika kituo cha polisi.
Akisimulia tukio hilo baada ya kuachiwa jijini Arusha leo Sep,1,2026, Malisa alianza kwa kuwashukuru Watanzania waliopaza sauti kuhusu kukamatwa kwake, akisema taarifa na kelele zilizotolewa na wananchi zilimpa matumaini na, kwa maelezo yake, zilisaidia kuhakikisha suala lake linafahamika kwa umma.
“Pengine kama siyo sauti ambayo imepaza Watanzania, labda usingekuwa hapa,” alisema.
Nairobi: Safari ya ndege yavurugika
Malisa alisema baada ya kurejea kutoka Marekani alifika Nairobi nchini Kenya, akiwa na mpango wa kuendelea na safari kwa ndege hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Hata hivyo, safari hiyo ilivurugika baada ya kutokea mgomo wa wafanyakazi katika sekta ya usafiri wa anga nchini Kenya.
Alisema ndege yake iliyokuwa ipae saa tano asubuhi ilichelewa na baadaye safari hiyo ikaahirishwa tena kutokana na kutokujulikana muda ambao mgomo huo ungeisha.
Kwa sababu hiyo, alilazimika kubadilisha mpango wa safari.
“Wakaniambia wanatusaidia kufanya tiketi yangu iwe open, maana yake naweza kuitumia wakati mwingine,” alisema.
Baada ya kushindwa kuendelea kwa ndege, Malisa alisema alitafuta usafiri wa gari binafsi kutoka Nairobi kuelekea Tanzania, akilenga kuingia nchini kupitia Namanga.
Namanga: Pasipoti yakwama
Alisema walipofika Namanga, upande wa Kenya pasipoti yake ilisomwa bila tatizo, lakini alipofika upande wa Tanzania akaambiwa pasipoti yake haisomeki na alitakiwa kusubiri.
Muda wa kusubiri uliongezeka, huku akiwa hajui kinachoendelea.
“Upande wa Kenya pasipoti ilisomwa, lakini upande wa Tanzania nikaambiwa pasipoti haisomeki, nisubiri,” alisema.
Malisa alisema baada ya kusubiri kwa muda, walifika watu waliojitambulisha kuwa ni polisi na kuwachukua kwa gari ambalo, kwa maelezo yake, halikuwa gari la polisi, ingawa waliambiwa lilikuwa linatumika kwa kazi hiyo.
Walielezwa kwamba wangepelekwa Kituo cha Polisi Longido.
Hapo ndipo, kwa mujibu wa simulizi yake, safari ilianza kuchukua sura nyingine.
‘Tulipita Longido’
Malisa alisema walishangaa baada ya gari walilokuwa wamepanda kuendelea na safari na kupita Longido badala ya kufika kituoni walikoambiwa.
“Wakati tunakuja tukafika Namanga... tukachukuliwa na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi. Gari haikuwa ya polisi, lakini ilitajwa kwamba ni ya polisi. Wakatwambia tutapelekwa kituo cha polisi Longido, lakini hawakutupeleka Longido,” alisema.
Badala yake, walifikishwa katika Kituo cha Polisi cha Diplomasia na Utalii jijini Arusha.
Malisa alisema yeye na watu wengine waliokuwa wamekamatwa katika mazingira tofauti waliwekwa katika kituo hicho.
Usiku mmoja kituoni
Kwa mujibu wa Malisa, walifika kituoni hapo na kulala hadi asubuhi.
Amesema licha ya mazingira ya tukio hilo na sintofahamu iliyokuwapo kuhusu alipo, hakupigwa wala kufanyiwa vitendo vya ukatili.
“Kwa kweli hapana. Hakukuwa na harassment yoyote. Hatukupigwa, hatukufanywa vitendo vyote vya ukatili,” alisema.
Alisema waliambiwa tu kwamba walihitajika kituoni kwa ajili ya kutoa maelezo.
Hata hivyo, anasema hakuelezwa tuhuma yoyote ya jinai dhidi yake.
‘Sikuhojiwa, sikusomewa tuhuma’
Malisa alisema baada ya kufikishwa kituoni, hakufanyiwa mahojiano kuhusu tuhuma yoyote ya jinai, wala hakusomewa kosa alilodaiwa kulifanya.
Badala yake, alielekezwa kuandika historia ya tukio la kukamatwa kwake.
“Niliambiwa niandike historia; jinsi nilivyokamatwa pale Namanga mpaka kufikishwa hapa. Ndiyo jambo nililoandika,” alisema.
Alisema simu yake, fedha, begi na vitu vingine alivyokuwa navyo vilibaki salama na vyote vilirudishwa baada ya kuachiwa.
Wakili naye apambana kutafuta alipo
Malisa alisema wakati yeye akiwa ameshikiliwa, wakili wake alikuwa akitafuta taarifa kuhusu alipo katika vituo mbalimbali vya polisi.
Amesema hali hiyo iliongeza wasiwasi kutokana na kwamba waliomchukua Namanga walidai kuwa ni polisi na walieleza kwamba wangempeleka Longido, lakini hakufikishwa huko.
“Wakili wangu jana amezunguka sana kwenye vituo vya polisi na karibu kila kituo walikuwa wanamwambia huyu mtu hatuna taarifa zake,” alisema.
Kwa maelezo yake, hali hiyo ilileta mkanganyiko mkubwa kuhusu mahali alipokuwa.
Asubuhi: Mlango wa uhuru wafunguka
Baada ya kulala kituoni usiku mmoja, Malisa alisema asubuhi taratibu zilifanyika na hatimaye akaachiwa huru.
Anasisitiza kwamba hakuachiwa kwa dhamana kwa sababu hakudhaminiwa wala kujidhamini, bali aliachiwa bila kufunguliwa mashtaka.
“Kwa maana kwamba mimi nilikamatwa, lakini asubuhi tumeachiwa huru. Sijadhaminiwa wala sijajidhamini,” alisema.
Malisa: Hili ni somo kwa Tanzania
Baada ya tukio hilo, Malisa amesema tukio hilo linapaswa kuwa zaidi ya suala lake binafsi, likawa nafasi ya kutafakari namna mfumo wa haki jinai unavyofanya kazi nchini.
Amesema kama mtu anayefahamika na mwenye uwezo wa kupata msaada wa jamii anaweza kushikiliwa bila kuelezwa tuhuma, ipo haja ya kujiuliza hali ya wananchi ambao hawana sauti au watu wa kuwasemea.
“Kwa hiyo kama huyu Malisa ambaye jamii inamwona na imetafsiriwa na imemkosoa maana ya kumtetea, ameweza kutendwa hivi bila kosa lolote, bila tuhuma zozote, bila jinai, ameweza kukamatwa akashikiliwa tu mahali halafu asubuhi akaambiwa nenda,” alisema.
Akaongeza:
“Maana yake wasio na sauti kama Malisa wanafanywa mangapi na nani atakuwa msemaji wao?”
‘Polisi wafanye kazi kwa weledi’
Malisa ameitaka Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi kwa weledi, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kujenga imani ya wananchi.
“Vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi kwa weledi. Vitasaidia pia kuongeza imani kwa wananchi,” alisema.
Amesema tukio lake limeonyesha umuhimu wa kuboresha mifumo ya haki jinai ili kuhakikisha mtu anayekamatwa anajulishwa sababu ya kukamatwa kwake na taratibu za kisheria zinafuatwa.
Kwa sasa, Malisa amesema hana taarifa ya tuhuma yoyote inayomkabili kutokana na tukio hilo, huku akisema inawezekana tuhuma zikaja baadaye.
“Labda tuhuma zije kuanzia sasa na kuendelea,” alisema.
Safari iliyokuwa imeanza kama kurejea nyumbani baada ya miezi kadhaa nchini Marekani, hivyo, kwa Malisa, iliishia kuwa usiku wa sintofahamu—kuanzia ndege iliyokwama Nairobi, kuvuka mpaka kwa gari, kusubiri Namanga, kuchukuliwa na watu waliojitambulisha kuwa polisi, kupelekwa Arusha badala ya Longido, kulala kituoni na hatimaye kuachiwa bila kusomewa tuhuma za jinai.
Ends


Post a Comment