RUTO AWAPIGA STOP WAGENI KUFANYA BIASHARA KENYA
.....Aagiza wafanyabiashara wa kigeni kuondoka sekta ya uchuuzi na maduka madogo, asema biashara hizo ni za Wakenya
By Arushadigital|NAIROBI, KENYA
RAIS wa Kenya, William Ruto, ameagiza serikali kuanza kuchukua hatua dhidi ya raia wa kigeni wanaojihusisha na biashara ndogo ndogo, uchuuzi na uendeshaji wa maduka madogo nchini humo, akisisitiza kuwa shughuli hizo zinapaswa kuwanufaisha Wakenya.
Ruto ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wafanyabiashara wa biashara ndogo, ndogo na za kati (MSMEs) katika Ikulu ya Nairobi, ambapo alisema serikali haitaruhusu wageni kuingia katika biashara ndogo na kushindana moja kwa moja na wafanyabiashara wa Kenya.
Alisema hatua za kiutawala dhidi ya raia wa kigeni wanaojihusisha na shughuli hizo zitaanza Jumatatu, Septemba 7, 2026, kabla hata ya kukamilika kwa mchakato wa kutunga sheria unaolenga kuweka kisheria masharti hayo.
Rais Ruto alieleza kuwa Kenya bado iko wazi kwa wawekezaji wa kigeni, lakini uwekezaji huo unapaswa kulenga shughuli zinazoongeza uzalishaji, kutengeneza ajira na kuchangia uchumi, badala ya wageni kuingia katika uchuuzi na biashara ndogo zinazoweza kufanywa na Wakenya.
Akizungumzia suala la raia wa China, Ruto alisema Kenya haiwezi kukubali mtu kutoka China au nchi nyingine kuingia nchini kwa ajili ya kufanya uchuuzi au kufungua duka dogo na kushindana na wafanyabiashara wa ndani.
“Haiwezi kuwa mtu anatoka China au sehemu nyingine kuja kuwa mchuuzi au kufungua duka dogo,” alisema Ruto, akisisitiza msimamo wake wa kulinda wafanyabiashara wa Kenya.
Rais huyo pia amesema kuna Muswada wa Biashara unaoshughulikiwa na Bunge unaopendekeza kuweka baadhi ya shughuli za biashara kuwa za Wakenya pekee na kuzuia raia wa kigeni kujihusisha nazo.
Aidha, Ruto ameliagiza Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda kuanza utekelezaji wa hatua hizo, huku akimtaka Waziri anayehusika na viongozi wa Bunge kuhakikisha muswada huo unashughulikiwa kwa haraka.
Katika hatua nyingine, Rais Ruto ameitaka Wizara ya Uhamiaji na mamlaka husika kuchunguza masharti na taratibu zinazotumika kuwapa raia wa kigeni vibali vya kuingia nchini kwa ajili ya kufanya biashara.
Amesema hatua hizo zinalenga kuhakikisha kuwa vibali vya uwekezaji na biashara vinatolewa kwa kuzingatia sheria na kwamba wageni hawatumii mianya ya kisheria kuingia katika shughuli ndogo zinazolenga kulindwa kwa ajili ya raia wa Kenya.
Ruto amesema hatua hiyo si ya kufunga milango kwa wawekezaji wa kigeni, bali ni kuhakikisha uwekezaji wa kigeni unaleta ajira na thamani kwa uchumi wa Kenya, huku wafanyabiashara wadogo wa ndani wakilindwa dhidi ya ushindani unaoweza kuwaathiri.
Ends

إرسال تعليق