KIMOTCO YAINGIZA MABASI MAPYA KWA AJILI YA AFCON 2027, YATOA AJIRA 60
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Benedict John Beresero, amesema Kimotco imeweka mkakati maalumu wa usafirishaji unaolenga kurahisisha safari za wageni na Watanzania wakati wa mashindano hayo, huku ikitoa huduma zinazokwenda sambamba na mahitaji ya watalii na mashabiki wa soka.
Amesema mpango huo unahusisha huduma ya usafiri, malazi na usafirishaji wa wageni hadi kwenye viwanja vya michezo, ambapo mteja atakapoweka booking ya usafiri kupitia kampuni hiyo, atawezeshwa pia kupata huduma za booking za hoteli pamoja na usafiri wa kwenda uwanjani.
“Tumeyaleta mabasi haya mahususi kwa ajili ya maandalizi ya AFCON 2027. Mteja akipanda basi letu au kufanya booking nasi, tutamsaidia pia kufanya booking ya hoteli na usafiri wa kumpeleka uwanjani,” amesema Beresero.
Amesema huduma hiyo haitakuwa kwa jiji la Arusha pekee, bali kampuni itahudumia maeneo mbalimbali ambayo mabasi yake yanafanya safari, ikiwamo Musoma, Tarime, Dodoma, Iringa, Njombe, Sumbawanga, Mbeya, Tunduma na Dar es Salaam.
AJIRA 60 KWA VIJANA
Amesema kwa sasa kampuni imefanikiwa kutoa ajira zinazokadiriwa kufikia 60, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mchango wa sekta binafsi katika juhudi za Serikali kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana.
“Tumejali sana suala la ajira. Mabasi haya takribani 20 yameweza kutoa ajira karibu 60 kwa vijana ambao walikuwa wanazunguka mtaani. Kwa kushirikiana na Serikali tumeweka ajira hizi ili kuisapoti Serikali,” amesema.
Amesema kampuni hiyo pia imejipanga kuhakikisha huduma kwa abiria inakuwa ya kiwango cha juu kwa kutumia madereva wenye uzoefu wa safari ndefu, miteremko na barabara zenye changamoto, huku makondakta wakipewa msisitizo wa kuwa na nidhamu na ustaarabu katika kuwahudumia abiria.
MABASI MAPYA TISA
Akieleza kuhusu uwekezaji huo, Beresero amesema kampuni imeingiza mabasi mapya tisa kwa awamu hiyo, yenye huduma za kisasa ikiwamo vyoo, Wi-Fi pamoja na burudani kupitia Azam TV.
Amesema mabasi hayo yataendelea kuimarisha mtandao wa usafiri wa Kimotco kutoka Arusha kwenda mikoa mbalimbali nchini, huku kampuni ikitarajia kupokea mabasi mengine 11 kabla ya mwisho wa mwaka 2026, na kufikisha jumla ya mabasi 20 katika mpango huo.
“Leo tumeingiza mabasi tisa mapya ya kisasa yenye huduma ya choo, Wi-Fi na Azam TV. Tunategemea kupokea magari mengine 11 na kufikisha jumla ya magari 20 ifikapo mwisho wa mwaka huu,” amesema.
Amesema baada ya kufikisha idadi hiyo, kampuni itaendelea kupanua mtandao wake kulingana na mahitaji ya abiria na wageni watakaokuwa nchini wakati wa AFCON 2027.
HUDUMA KWA WANAFUNZI
Mbali na huduma za safari za kawaida na maandalizi ya AFCON, Kimotco pia imejikita katika kutoa huduma za usafiri kwa wanafunzi, huku kampuni ikitoa mfumo wa tiketi za mtandaoni.
Beresero amesema huduma hiyo inalenga kuwapa wazazi uhakika wa usalama na usafiri wa watoto wao wanapokuwa wakisafiri kwenda au kutoka mikoa mbalimbali inayohudumiwa na kampuni hiyo.
“Tunatoa huduma kwa wanafunzi kwenye shule mbalimbali na tunakata tiketi online. Tunamhakikishia mzazi kwamba mtoto wake akifika Kimotco katika mikoa tuliyotaja atafika nyumbani bila mzazi kulazimika kumfuatilia,” amesema.
Amesema Kimotco itaendelea kuwekeza katika mabasi, teknolojia na rasilimali watu ili kuhakikisha inakuwa sehemu ya maandalizi ya mafanikio ya Tanzania katika kuandaa na kuendesha AFCON 2027.
AFCON 2027 inatarajiwa kufanyika kwa pamoja nchini Tanzania, Kenya na Uganda, huku maandalizi ya miundombinu, usafiri, malazi na huduma nyingine muhimu yakiendelea katika nchi hizo.
Ends..











Post a Comment