CHEM CHEM YATWAA TENA TUZO YA HOTELI BORA YA KIFAHARI AFRIKA
Na Joseph Ngilisho | MANYARA
HOTELI ya kitalii ya Chem Chem Safari Lodge, iliyopo katika eneo la Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori (WMA) Burunge, Wilaya ya Babati mkoani Manyara, imeandika historia mpya kwa kutwaa kwa mara ya pili mfululizo tuzo ya Hoteli Bora ya Kifahari Barani Afrika, inayotolewa na taasisi ya kimataifa ya utalii ya World Travel Awards (WTA).
Ushindi huo umeifanya Chem Chem Safari Lodge kutwaa tuzo hiyo kwa miaka miwili mfululizo, baada ya kufanya hivyo mwaka 2025 na 2026, sambamba na kutambuliwa pia kama Lodge Bora ya Kifahari Tanzania.Mafanikio hayo yanaelezwa kuwa ni matokeo ya mkakati wa muda mrefu wa waanzilishi wa Chem Chem, Nicholas Negri na Fabia Bausch, ambao wameweka mkazo katika kuifanya Burunge WMA kuwa miongoni mwa maeneo bora ya uhifadhi na utalii wa kifahari barani Afrika.
Mkakati huo unahusisha utoaji wa huduma za kiwango cha juu kwa watalii, uhifadhi na ongezeko la wanyamapori, ulinzi wa mazingira pamoja na kuhakikisha jamii zinazozunguka eneo hilo zinashirikishwa katika shughuli za utalii na uhifadhi.
Akizungumza baada ya Chem Chem kukabidhiwa tuzo hizo, Meneja Mkuu wa Chem Chem Safari Lodge, Jorg Weytjens, alisema ushindi huo ni uthibitisho wa imani ambayo watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani wameendelea kuwa nayo kutokana na huduma wanazopata katika hoteli hiyo.“Tunawashukuru sana watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa kuendelea kutupigia kura na kutupa ushindi kutokana na huduma bora tunazotoa,” alisema Weytjens.
Alisema mafanikio hayo yataendelea kuwapa hamasa wafanyakazi wa Chem Chem kuongeza ubora wa huduma na kuhakikisha watalii wanaendelea kupata uzoefu wa kipekee wanapofika Burunge.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Anna Mbogo, alisema ushindi huo ni kielelezo cha ushirikiano uliopo kati ya Serikali, wananchi wa vijiji 10 vinavyounda eneo hilo la WMA na Chem Chem.
“Sisi kama Serikali tunapongeza ushindi huu kwani utaendelea kuitangaza Wilaya yetu ya Babati, kuongeza mapato na kutimiza dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuvutia watalii nchini Tanzania,” alisema Mbogo.
Alisema kutambuliwa kwa Chem Chem katika ngazi ya Afrika kunaongeza thamani ya Babati na Manyara kwa ujumla katika ramani ya utalii wa kimataifa, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali, wawekezaji na jamii.
Meneja wa Rasilimali Watu wa Chem Chem, Jennifer Giray, alisema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa wa uongozi katika rasilimali watu, mazingira ya kazi na ubora wa huduma.
“Tunawashukuru sana wakurugenzi wetu Nicholas na Fabia kwa usimamizi mzuri na malengo makubwa waliyotuandalia. Sasa tunaona matokeo yake, kwani tunafanya vizuri Afrika,” alisema Giray.
Alisema wafanyakazi wa Chem Chem wamekuwa wakifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa, jambo ambalo limekuwa msingi wa utoaji wa huduma bora na mazingira rafiki kwa wageni.
Naye Muongoza Watalii wa Chem Chem, Isack Joseph, alisema wanajivunia kutambuliwa kwa kazi wanayoifanya na kuahidi kuendelea kuboresha huduma ili kuvutia watalii wengi zaidi kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Joseph alisema ongezeko la watalii litasaidia kuongeza mapato kwa hoteli, jamii zinazozunguka eneo hilo pamoja na Serikali kupitia shughuli mbalimbali zinazohusiana na utalii.
Meneja wa Huduma wa Chem Chem, George Andrew, alisema lengo lao kubwa ni kuhakikisha kila mtalii anayefika katika hoteli hiyo anapata huduma bora na uzoefu wa kipekee.
Alisema ushirikiano wanaoupata kutoka Serikali kuanzia ngazi ya Taifa hadi vijijini umechangia kwa kiasi kikubwa kuweka mazingira salama na rafiki kwa watalii wanaotembelea eneo hilo.
“Tunathamini sana ushirikiano tunaoupata kutoka Serikali kuanzia ngazi ya Taifa hadi vijijini. Ushirikiano huu unatufanya tuweze kuwahudumia watalii katika mazingira salama na kuwafanya wajisikie furaha wakati wote wanapokuwa hapa,” alisema Andrew.
Ushindi wa Chem Chem ulitangazwa katika hafla ya utoaji wa tuzo za World Travel Awards iliyofanyika Zanzibar wiki iliyopita, ambapo Tanzania iliendelea kuonekana katika nafasi muhimu kwenye ramani ya utalii wa kimataifa.
Kwa kutwaa tuzo hiyo kwa mara ya pili mfululizo, Chem Chem Safari Lodge imeendelea kujijengea nafasi kama moja ya maeneo yanayoongoza kwa utalii wa kifahari barani Afrika, huku ushindi huo ukiipa Tanzania na Mkoa wa Manyara nafasi zaidi ya kutambulika kimataifa kama kituo muhimu cha utalii wa hali ya juu.
MWISHO





Post a Comment