MWANAHARAKATI MALISA GJ ‘AKAMATWA’ NAMANGA AKIINGIA NCHINI , HADI SASA HAJULIKANI ALIPO

MALISA GJ ‘AKAMATWA’ NAMANGA, ALIKOWAPI HAKUJULIKANI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MWANAHARAKATI Malisa GJ anadaiwa kukamatwa katika eneo la Namanga, mpakani mwa Tanzania na Kenya, huku hadi sasa kukiwa hakuna taarifa rasmi kuhusu alipo wala sababu za kushikiliwa kwake.

Madai hayo yametolewa na wakili Dickson Matata, ambaye amesema Malisa alikuwa akirejea nchini Tanzania kutoka Marekani, ambako alikuwa akiishi kwa zaidi ya miezi tisa kwa ajili ya mafunzo ya uongozi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wakili Matata, Malisa aliwasili Nairobi nchini Kenya jana asubuhi, lakini alishindwa kuendelea na safari yake kutokana na mgomo wa wafanyakazi katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Inadaiwa kuwa kutokana na hali hiyo, aliamua kutumia usafiri wa barabara hadi Namanga, mpakani mwa Kenya na Tanzania.

Wakili Matata amesema Malisa alipofika Namanga majira ya saa tisa mchana, alikwenda katika kituo cha Uhamiaji kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kuingia nchini.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, Malisa aliambiwa hati yake ya kusafiria haikusomeka katika mfumo na hivyo alitakiwa kusubiri mkuu wa kituo kwa ajili ya hatua zaidi.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa majira ya saa moja jioni, Malisa alichukuliwa na gari jeupe aina ya Double Cabin, ambalo kwa mujibu wa wakili huyo halikuwa na alama za Polisi, na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Longido.

Wakili Matata amedai kuwa baada ya hapo, gari hilo liliondoka kuelekea Arusha, huku simu za Malisa zikizimwa na mawasiliano naye kukatika.

Hali hiyo imeibua maswali kuhusu alipo mwanaharakati huyo na sababu za kushikiliwa kwake, huku wakili wake akitaka mamlaka husika kutoa ufafanuzi wa haraka.

Wakili Matata amezitaka Polisi na Uhamiaji kutoa taarifa rasmi kuhusu mahali alipo Malisa GJ, sababu za kushikiliwa kwake na kuhakikisha anapatiwa haki zake za kisheria.

Miongoni mwa haki hizo, amesema, ni pamoja na Malisa kuruhusiwa kuonana na mawakili wake na kupata fursa ya kuwasiliana na watu wake wa karibu kwa mujibu wa sheria.

Hadi habari hii inaandikwa, hakuna taarifa rasmi kutoka Jeshi la Polisi au Idara ya Uhamiaji iliyothibitisha madai ya kukamatwa au kushikiliwa kwa Malisa GJ, wala kutoa sababu za hatua hiyo.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم