Breaking🔥

DC KARATU AWATAKA WANANCHI KUTUMIA NYARAKA HALALI KUPATA NIDA

 DC KARATU AWATAKA WANANCHI KUTUMIA NYARAKA HALALI KUPATA NIDA

Na Joseph Ngilisho | KARATU

Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Dkt. Lameck Karanga, amewataka wananchi kutumia nyaraka halali na zenye taarifa sahihi wakati wa kujiandikisha kupata Namba na Vitambulisho vya Taifa (NIDA), akisema kufanya hivyo kutasaidia kupunguza changamoto katika mchakato wa usajili na utoaji wa vitambulisho.

Dkt. Karanga ametoa kauli hiyo jana, Septemba 1, 2026, alipofika katika Kijiji cha Qaru, Tarafa ya Endabash, Wilaya ya Karatu, kujionea zoezi la uandikishaji wa wananchi katika mfumo wa NIDA.

Amesema upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa ni muhimu kwa wananchi katika kupata huduma mbalimbali, hivyo ni muhimu kila mwananchi kuhakikisha anawasilisha taarifa sahihi na nyaraka zinazotambulika kisheria wakati wa usajili.



“Wananchi wanapaswa kuhakikisha wanatumia nyaraka halali na sahihi wakati wa kuwasilisha taarifa zao. Hii itasaidia kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza katika usajili na utoaji wa namba pamoja na Vitambulisho vya Taifa,” amesema Dkt. Karanga.

Mkuu huyo wa Wilaya pia ameupongeza uongozi wa NIDA kwa kupeleka huduma hiyo karibu na wananchi, hususan katika maeneo ya vijijini ambako baadhi yao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za kufika katika vituo vya huduma.

Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha wananchi kupata huduma hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia fursa hiyo kuhakikisha wanapata nyaraka hizo muhimu.

Zoezi la uandikishaji katika Kijiji cha Qaru limefanyika kwa takribani siku mbili, huku jana ikiwa siku ya hitimisho la huduma hiyo katika eneo hilo.

Baada ya kukamilisha zoezi hilo Qaru, timu ya NIDA inatarajiwa kuendelea na uandikishaji katika maeneo mengine yenye changamoto, kwa lengo la kuwafikia wananchi ambao bado hawajapata Namba au Vitambulisho vya Taifa.

Hatua hiyo inalenga kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za NIDA kwa wananchi, hasa wale wanaoishi katika maeneo ya vijijini na ambayo huduma hizo zimekuwa hazipatikani kwa urahisi.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم