Breaking🔥

BODI YANG'AKA YAMREJESHA MADARAKANI KATIBU MKUU TWARIQA, SHEIKH HARUNA HUSEIN ,YATOA ONYO KALI KWA MWENYEKITI ...'ALICHUKUA MAAMUZI KIHUNI'

BODI YANG'AKA, YAMREJESHA MADARAKANI KATIBU MKUU TWARIQA, SHEIKH HARUNA HUSEIN ,YATOA ONYO KALI KWA MWENYEKITI

Na Joseph Ngilisho | ARUA

BODI ya Wadhamini ya Taasisi ya Kiislamu ya Twariqa Qadiriyya Al-Razouqia Tanzania imemrejesha madarakani Katibu Mkuu wa Taifa, Sheikh Haruna Husein, baada ya kubaini kuwa uamuzi wa kumuondoa katika nafasi hiyo haukufuata taratibu za taasisi, huku ikimpa onyo kali Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Sheikh Salimu Mubaraka.

Bodi hiyo imesema mamlaka ya kuchukua hatua dhidi ya viongozi wa taasisi hiyo yanapaswa kutekelezwa na chombo chenye dhamana kwa mujibu wa Katiba , kanuni na taratibu zilizowekwa , na kwamba hakuna kiongozi mmoja anayepaswa kujichukulia mamlaka ya kufanya maamuzi makubwa bila kuwashirikisha wahusika wenye mamlaka.

Akizungumza mapema leo Sep 5,2026  kuhusu uamuzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Shaffi Ali Mkande, amesema baada ya kulijadili suala la kuondolewa kwa Sheikh Haruna kwa kina, Bodi ilibaini kuwepo kwa ukiukwaji wa utaratibu na hivyo kuamua kumrejesha rasmi katika nafasi yake.

“Bodi imejadili suala hili na kuona kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa utaratibu katika kumuondoa Katibu Mkuu. Kwa hiyo, tunatangaza kwamba Sheikh Haruna Husein anaendelea na nafasi yake ya Katibu Mkuu wa Taifa,” amesema Mkande.

Amesema viongozi wote wanapaswa kuheshimu mipaka ya mamlaka yao na kuhakikisha maamuzi yanayohusu taasisi yanafanyika kwa kuzingatia Katiba, kanuni na misingi ya dini.

Bodi pia imemtaka Sheikh Salimu Mubaraka kuacha kujichukulia mamlaka na kusisitiza kuwa uongozi wa taasisi hauwezi kuendeshwa kwa maamuzi ya mtu mmoja bila kushirikisha vyombo vilivyopewa dhamana.

ULAMAA WAKATAA KUSIMAMISHWA KWA KATIBU

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulamaa wa Twariqa, Salim Muhonzi, amesema Baraza la Mashauri haliwezi kuunga mkono hatua ya kumsimamisha Katibu Mkuu kwa kuwa haikuzingatia misingi ya mashauriano inayosisitizwa katika Uislamu.

Muhonzi amesema maamuzi yanayohusu taasisi yanapaswa kufanywa baada ya viongozi husika kukaa pamoja, kushauriana na kufikia uamuzi kwa kuzingatia Katiba na misingi ya Qur’ani.

“Katika dini, tunapotaka kufanya jambo lazima tushauriane. Mashauriano kwanza, kisha ndiyo tufanye lile jambo,” amesema.

Amesema kutokuwepo kwa mashauriano ndiko kulikosababisha mvutano uliopo, akisisitiza kuwa hata Katiba ya taasisi iliyotungwa na binadamu inapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia misingi ya Qur’ani.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini, Rehema Athuman, amesema Bodi haitambui matamko yaliyotolewa nje ya mamlaka ya kikatiba kuhusu kusimamishwa au kuondolewa kwa viongozi wa taasisi hiyo.

Amesema mamlaka ya kushughulikia masuala ya viongozi yako chini ya vyombo vilivyowekwa na taasisi, hivyo matamko yanayotolewa bila kufuata utaratibu hayawezi kuwa na uhalali wa kiuongozi.

“Sisi kama Bodi ya Wadhamini hatutambui tamko lile. Waliotangaza hawakuwa na mamlaka ya kufanya hivyo, kwa sababu mwenye mamlaka ya kutoa tamko kama hilo anajulikana,” amesema Athuman.

Athuman amewataka viongozi wa dini kutumia nafasi zao kuimarisha amani na utulivu, akisisitiza kuwa hawapaswi kutoa kauli au kuchukua hatua zinazoweza kuongeza taharuki katika jamii.

Amesema Bodi iko tayari kukemea vitendo vinavyoweza kuvuruga amani na mshikamano, huku ikisisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kushirikiana katika kutatua tofauti kwa njia ya mazungumzo na mashauriano.

Uamuzi wa Bodi wa kumrejesha Sheikh Haruna Husein sasa umeweka wazi mgawanyiko wa kimamlaka ndani ya taasisi hiyo, huku viongozi wa Bodi na Ulamaa wakisisitiza kuwa Katiba, mashauriano na taratibu za taasisi lazima zitumike katika kutatua mvutano huo.

...Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم