...DEREVA ALIKUWA AKIFUNDISHWA KUWEKA GIA.. AINGIA AJALI KING'ORI
MMOJA AFARIKI, WAWILI WAJERUHIWA; BASI YATEKETEA KWA MOTO
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
ABIRIA wa basi lililohusika katika ajali iliyosababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi wawili eneo la Kingori, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, amesema walikuwa na hofu na namna dereva wa basi hilo alivyokuwa akiendesha muda mfupi kabla ya ajali hiyo.
Abiria huyo amesema hofu hiyo iliongezeka baada ya kubaini kuwa dereva alikuwa akipewa maelekezo ya namna ya kuendesha na mtu aliyekuwa ameketi pembeni yake, hali iliyowafanya baadhi ya abiria kutamani kulisimamisha basi na kutoa taarifa kwa askari wa usalama barabarani.
Kwa mujibu wa abiria huyo, mtu aliyekuwa pembeni ya dereva alikuwa akimwelekeza namna ya kuingia barabarani na wakati mwingine kumpongeza baada ya kutekeleza maelekezo hayo.
“Alikuwa anaonekana kama mtu anayejifunza kuendesha. Yule aliyekuwa pembeni yake alikuwa akimuelekeza, akimwambia aingie vizuri barabarani, halafu anasema ‘vizuri sana’,” amesema abiria huyo.
Amesema hali hiyo iliwafanya abiria kuwa na wasiwasi na kutamani kufika eneo ambalo wangekutana na askari wa usalama barabarani ili waweze kutoa taarifa kuhusu mwenendo wa dereva.
Hata hivyo, amesema kabla hawajafikisha taarifa hiyo kwa askari, basi hilo liligongana uso kwa uso na gari aina ya Alphard katika eneo la Kingori, barabara ya Arusha–Moshi.
BASI LATEKETEA
Ajali hiyo imetokea jana, Agosti 8, 2026, majira ya saa 4:30 asubuhi, ikihusisha basi aina ya Scania lenye namba za usajili T 639 AQN, lililokuwa likitokea Arusha kuelekea Tanga, na gari aina ya Alphard lenye namba T 837 EMS, lililokuwa likitokea Kilimanjaro kuelekea Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, amesema baada ya magari hayo kugongana yaliwaka moto, huku mtu mmoja aliyekuwa ndani ya Alphard akifariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa.
Amesema marehemu ni raia wa kigeni, huku majeruhi wakikimbizwa kwa ajili ya kupata matibabu.
“Ajali hiyo imetokea Agosti 8 mwaka huu, majira ya saa 4:30 asubuhi. Magari yote mawili yaligongana na baada ya hapo yaliwaka moto, na kusababisha kifo cha abiria mmoja ambaye ni raia wa kigeni na majeruhi wawili waliokuwa kwenye gari ndogo,” amesema Masejo.
ABIRIA WAOKOLEWA
Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Arusha, SSF Osward Mwanjejele, amesema baada ya kupokea taarifa za ajali hiyo, askari wa zimamoto na uokoaji waliwasili eneo la tukio na kufanya operesheni ya kuwaokoa waliokuwa ndani ya magari hayo.
Amesema walifanikiwa kuwaokoa abiria wote waliokuwa ndani ya basi pamoja na majeruhi wawili waliokuwa kwenye gari ndogo, huku wakifanikiwa pia kudhibiti na kuzima moto uliokuwa ukiendelea kuteketeza magari hayo.
POLISI WACHUNGUZA
Kamanda Masejo amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo.
Ametoa wito kwa madereva wote kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua hatua dhidi ya madereva watakaobainika kukiuka sheria.
Uchunguzi wa Polisi unatarajiwa kubaini mazingira yaliyosababisha magari hayo kugongana, wakati ushuhuda wa abiria ukieleza kuwa kulikuwa na hali ya wasiwasi kuhusu namna basi hilo lilivyokuwa likiendeshwa kabla ya ajali.
Ends


إرسال تعليق