WATOTO 95% ARUMERU MAGHARIBI WAATHIRIKA NA FLUORIDE; DAKTARI BINGWA AONYA HATARI YA MGOGORO WA AFYA YA MENO

 Na Joseph Ngilisho | ARUMERU


UCHUNGUZI wa awali uliofanywa kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Ngaramtoni, Wilaya ya Arumeru, umebaini kuwa karibu asilimia 95 ya watoto wameathirika na kiwango kikubwa cha madini ya fluoride kwenye meno yao, hali inayofahamika kitaalamu kama Dental Fluorosis, jambo lililowaibua wataalamu kutaka hatua za haraka zichukuliwe kukabiliana na tatizo hilo.

Akizungumza  wakati wa zoezi la utoaji wa huduma za afya ya kinywa na meno katika kata shule ya msingi Nduruma linaloendelea katika Jimbo la Arumeru Magharibi kwa ushirikiano wa madaktari bingwa kutoka Ujerumani, Daktari Bingwa wa Afya ya Kinywa na Meno, Dkt. Ibrahim Kassambala, alisema ukubwa wa tatizo hilo unaonyesha wazi kuwa athari za fluoride katika ukanda huo ni kubwa kuliko ilivyodhaniwa.

Dkt. Kassambala, ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mkufunzi wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Mbeya na daktari bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya

 Alisema timu hiyo ikiongozwa na daktari bingwa wa Afya ya Kinywa na Meno kutoka ujerumani dkt. Ursula Suessbier ipo Arusha kwa msaada wa Mbunge wa Arumeru Magharibi Dkt Johannes Lukumay kwa ajili ya kampeni ya siku saba ya Dental Outreach inayojumuisha elimu, uchunguzi na matibabu ya afya ya kinywa na meno katika shule za msingi, vituo vya watoto yatima, Sober House na Hospitali ya Seliani.

"Tupo Arusha kwa ajili ya huduma za outreach za afya ya kinywa na meno katika shule za msingi, lakini pia tutakwenda Sober House, Orphanage Centre na Hospitali ya Seliani kama sehemu ya huduma kwa jamii," alisema.

Alisema uchunguzi uliofanyika Ngaramtoni umeonyesha watoto wengi wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ya afya ya kinywa na meno ikiwemo meno yaliyotoboka, magonjwa ya fizi na mpangilio usio sahihi wa meno.Hata hivyo, alisema kilichowashtua zaidi ni ukubwa wa athari za fluoride.

"Watoto karibu asilimia 95 meno yao yameathirika na kiwango kikubwa cha fluoride. Wapo wenye kiwango kidogo, cha kati na wengine kiwango kikubwa kabisa cha Dental Fluorosis," alisema.

Kwa mujibu wa Dkt. Kassambala, hali hiyo inaonyesha kuwa tatizo la fluoride katika Arumeru linahitaji mkakati wa kitaifa unaojumuisha wataalamu wa afya, sekta ya maji na mamlaka nyingine husika.

Aliwataka wazazi kupunguza matumizi ya vyakula na vinywaji vyenye sukari nyingi kwa watoto, kuhakikisha wanapiga mswaki angalau mara mbili kwa siku kwa kutumia dawa ya meno inayoshauriwa na wataalamu na kuwapeleka watoto kupimwa afya ya kinywa na meno angalau mara mbili kwa mwaka.

"Tunashauri wazazi wajenge utamaduni wa kuwapeleka watoto kuchunguzwa mara mbili kwa mwaka ili matatizo yabainike mapema na yatibiwe kabla hayajawa makubwa," alisema.

Kuhusu kiwango kikubwa cha fluoride kwenye maji, alisema wataalamu watakabidhi matokeo ya uchunguzi kwa mamlaka husika ili kutafutwa suluhisho la kudumu, likiwemo matumizi ya teknolojia za kisasa za kutibu maji na kupunguza kiwango cha fluoride kabla hayajatumika na wananchi.

"Kuna teknolojia za kisasa za kutibu maji katika ngazi ya jamii ambazo zinaweza kusaidia kuhakikisha kiwango cha fluoride kinakuwa salama kwa matumizi ya binadamu," alisema.

Wakati huo huo, Diwani wa Kata ya Nduruma, Samweli Menavi, amesema tatizo la afya ya kinywa na meno katika kata hiyo ni kubwa na linaaminika kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na maji yanayotumiwa na wananchi.

Menavi alisema ujio wa madaktari bingwa kutoka Ujerumani kwa kushirikiana na madaktari wa Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru ni tukio la kihistoria kwa wananchi wa Nduruma.

"Kwa mara ya kwanza tangu nikiwa mdogo nimeshuhudia madaktari bingwa kutoka nje ya nchi wakifika katika Kata ya Nduruma kutoa elimu na huduma za afya ya kinywa na meno. Hili ni jambo kubwa sana kwa wananchi wetu," alisema.

Alisema licha ya wananchi wengi kujitahidi kufanya usafi wa kinywa, changamoto ya ubora wa maji imeendelea kuchangia kuongezeka kwa matatizo ya meno, hivyo elimu inayotolewa pamoja na matibabu inapaswa kuambatana na juhudi za kuboresha huduma za maji.

"Tunaamini maji tunayoyatumia yana mchango mkubwa katika tatizo hili. Tunahitaji suluhisho la kudumu la kuboresha ubora wa maji ili kupunguza athari hizi kwa wananchi," alisema.

Diwani huyo alimpongeza Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, kwa kuwezesha ushirikiano uliowaleta madaktari hao kutoka Ujerumani, akisema hatua hiyo imefungua ukurasa mpya wa kuboresha huduma za afya ya kinywa na meno katika jimbo hilo.

Aidha, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini Dkt. Lukumay katika nafasi yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya, akisema uongozi huo umeendelea kuleta manufaa yanayoonekana kwa wananchi.

Menavi alisema elimu inayotolewa kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Nduruma itawajengea uwezo wa kuwa mabalozi wa afya ya kinywa na meno katika familia zao, huku akitoa wito kwa serikali na wadau kuendelea kuwekeza katika utafiti, elimu, matibabu na miradi ya kuboresha ubora wa maji ili kupunguza mzigo wa magonjwa ya meno katika Arumeru Magharibi.








Ends..


Post a Comment

أحدث أقدم