MADAKTARI BINGWA WA UJERUMANI NA TANZANIA WABAINI THELUTHI MOJA YA WANAFUNZI NDURUMA WANA MATATIZO YA MENO
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
TIMU ya madaktari bingwa wa afya ya kinywa na meno ikiongozwa na Daktari Bingwa kutoka Ujerumani, Dkt. Ursula Suessbier, kwa kushirikiana na Daktari Bingwa wa Kitanzania, Dkt. Ibrahim Kassambala na madaktari wa halmashauri ya Arusha, imebaini kuwa takribani theluthi moja ya wanafunzi 546 wa Shule ya Msingi Nduruma, Wilaya ya Arumeru, wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ya afya ya kinywa na meno, yakiwemo meno yaliyotoboka, magonjwa ya fizi, ugaga na mpangilio usio sahihi wa meno.
Uchunguzi huo umefanyika ikiwa ni sehemu ya programu ya siku saba ya utoaji wa huduma za afya ya kinywa na meno inayotekelezwa na Asasi ya NEPT kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Tanzania na Ujerumani, kufuatia jitihada za Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, za kuleta huduma hizo kwa wananchi wa jimbo hilo.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa uchunguzi katika Shule ya Msingi Nduruma, Daktari Bingwa wa Afya ya Kinywa na Meno, Dkt. Ibrahim Kassambala, alisema timu hiyo inaundwa na madaktari kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Mbeya (MUST), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, madaktari wa Mkoa wa Arusha pamoja na wataalamu kutoka Ujerumani.
Alisema lengo la programu hiyo ni kuboresha afya ya kinywa na meno kwa makundi mbalimbali ya jamii kupitia utoaji wa elimu, uchunguzi na matibabu ya bure katika shule za msingi, vituo vya kurekebisha waathirika wa uraibu, vituo vya kulelea watoto yatima na kambi za matibabu zitakazofanyika Seliani na Ngaramtoni.
"Tumetoa elimu ya afya ya kinywa na meno kwa wanafunzi, tukiwafundisha namna sahihi ya kutunza meno yao ili yasitoboke, kujikinga dhidi ya magonjwa ya fizi na changamoto nyingine za afya ya mdomo. Baada ya hapo tumefanya uchunguzi wa afya zao za kinywa na meno," alisema Dkt. Kassambala.
Alisema uchunguzi umeonyesha watoto wengi wenye meno yaliyooza kutokana na kutoboka, wengine wenye magonjwa ya fizi yanayosababisha kutoka damu, huku wengine wakibainika kuwa na mpangilio mbaya wa meno pamoja na ugaga.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wazazi kuwapeleka watoto wao kliniki za afya ya kinywa na meno angalau mara mbili kwa mwaka hata kama hawana maumivu, akieleza kuwa uchunguzi wa mapema husaidia kugundua na kutibu matatizo kabla hayajafikia hatua kubwa.
Aidha, aliwashauri wazazi kuhakikisha watoto wanapiga mswaki mara mbili kwa siku, asubuhi na usiku, kwa kutumia dawa ya meno yenye madini ya fluoride, kupunguza matumizi ya vyakula vyenye sukari nyingi kama pipi, biskuti na ice cream, pamoja na kuwapatia miswaki na dawa bora za meno.
Katika kuhamasisha utunzaji wa afya ya kinywa na meno, timu hiyo iliwagawia wanafunzi miswaki na dawa za meno aina ya Colgate bila malipo.
Dkt. Kassambala alisema watoto waliobainika kuwa na matatizo makubwa yanayohitaji matibabu ya haraka tayari wameorodheshwa na wataanza kupatiwa matibabu siku za Alhamisi na Ijumaa baada ya wazazi wao kutoa ridhaa kupitia walimu wa shule.
Alieleza kuwa kutokana na idadi kubwa ya watoto wenye changamoto, si wote watakaohudumiwa katika awamu hiyo ya kwanza, hivyo waliobaki wataendelea kupatiwa huduma katika awamu nyingine za kambi ambazo zitafanyika katika miezi ijayo.
Kuhusu watoto wenye tatizo la mpangilio mbaya wa meno, Dkt. Kassambala alisema wataelekezwa katika kliniki maalumu za afya ya kinywa na meno mkoani Arusha kwa matibabu ya muda mrefu, akibainisha kuwa tatizo hilo linaweza kusababishwa na urithi au tabia kama kunyonya kidole na kutafuna vitu vigumu visivyokuwa chakula.
Alisema matibabu ya kurekebisha mpangilio wa meno yanahitaji muda mrefu wa ufuatiliaji pamoja na gharama kubwa, hivyo katika kambi hiyo jukumu kubwa ni kufanya uchunguzi, kutoa ushauri na kuwaunganisha wazazi na madaktari wa hapa Arusha kwa huduma endelevu.
Kwa mujibu wa Dkt. Kassambala, kati ya wanafunzi wapatao 500 wa Shule ya Msingi Nduruma waliofanyiwa uchunguzi, karibu theluthi moja walikutwa na changamoto za afya ya kinywa na meno, hali inayosisitiza umuhimu wa kuwekeza zaidi katika elimu ya kinga, uchunguzi wa mapema na huduma za afya ya kinywa kwa watoto wa shule za msingi.
Ends













إرسال تعليق