LUKUMAY AFICHUA SABABU YA KUWALETA MADAKTARI BINGWA WA UJERUMANI ARUMERU, AISHUKURU SELIANI KWA KUFANIKISHA KAMBI YA MENO
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, amesema ukubwa wa tatizo la afya ya kinywa na meno linalowakabili wananchi wa jimbo lake ndiyo uliomshawishi kutumia mtandao wa Ngorongoro Education Project Tanzania-UK (NEPT-UK) kuwakaribisha madaktari bingwa wa afya ya kinywa na meno kutoka Ujerumani kuja kutoa huduma za kibingwa na kushirikiana na wataalamu wa Tanzania.
Akizungumza na wafanyakazi wa Hospitali ya Seliani-Ngaramtoni baada ya kuhitimishwa kwa kambi ya siku mbili ya matibabu ya afya ya kinywa na meno, Dkt. Lukumay alisema tathmini zilizofanyika katika shule na jamii zimeonyesha kuwa watoto na wananchi wengi wanakabiliwa na matatizo ya meno yaliyotoboka, magonjwa ya fizi pamoja na athari za madini ya fluoride kwenye maji, hali iliyomlazimu kutafuta ushirikiano wa kimataifa ili kusaidia kukabiliana na changamoto hiyo.
Alisema kupitia Ngorongoro Education Project Tanzania-UK (NEPT-UK), walifanya mawasiliano na taasisi ya Dental Global ya Ujerumani na kufanikiwa kuwashawishi madaktari bingwa wakiongozwa na Dkt. Ursula Suessbier kufika Arumeru, ambako walitoa huduma za uchunguzi na matibabu kwa zaidi ya wananchi 1,500.
"Kutokana na ukubwa wa tatizo hili, tuliona ni muhimu kutafuta ushirikiano wa kimataifa. Kupitia NEPT-UK tulifanikiwa kuwaleta madaktari hawa ambao wamehudumia mamia ya wagonjwa na kuacha msingi mzuri wa ushirikiano wa muda mrefu," alisema Lukumay.
Alisema kabla ya kuanza kambi ya matibabu katika Hospitali ya Seliani-Ngaramtoni, timu hiyo ilitembelea Shule za Msingi Ngaramtoni na Nduruma, ambako ilitoa elimu ya usafi wa kinywa na meno, ikagawa miswaki na dawa za meno na kufanya uchunguzi uliobaini wanafunzi wengi wakiwa na meno yaliyotoboka, magonjwa ya fizi na athari za fluoride.
Dkt. Lukumay aliishukuru Hospitali ya Seliani-Ngaramtoni kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha katika kuwapokea madaktari hao, kuandaa mazingira ya kambi na kushirikiana nao kutoa huduma kwa wananchi.
"Niwapongeze viongozi, madaktari, wauguzi na watumishi wote wa Hospitali ya Seliani kwa ushirikiano wenu mkubwa. Mmeonyesha kiwango cha juu cha weledi na kujituma, jambo lililochangia mafanikio makubwa ya kambi hii. Bila ushirikiano wenu, mafanikio haya yasingewezekana," alisema.
Aliongeza kuwa madaktari hao wa Ujerumani wameondoka wakiwa wameridhishwa na ushirikiano walioupata kutoka kwa wataalamu wa Tanzania na wameahidi kurejea tena nchini kuendeleza huduma, kubadilishana uzoefu wa kitaaluma na kujadili uwezekano wa kuanzisha ushirikiano wa kudumu utakaowezesha kufunguliwa kwa kliniki ya kisasa ya afya ya kinywa na meno nchini.
Mbunge huyo alisema ataendelea kutumia NEPT-UK na wadau wengine wa maendeleo kuvutia miradi ya afya na elimu itakayoboresha huduma kwa wananchi wa Arumeru na Tanzania kwa ujumla.
Ends





Post a Comment