HOFU YATANDA SANAWARI YA JUU ARUSHA KUNDI LA VIJANA LAWATISHIO KWA UBAKAJI,WAMBAKA MLEMAVU WA AKILI NA KUTOWEKA ,TAARIFA YAFIKA POLISI WATUHUMIWA WAENDELEZA KUPETA MTAANI BILA KUKAMATWA

HOFU IMETANDA SANAWARI YA JUU, MOIVO BAADA YA BINTI MWENYE ULEMAVU WA AKILI, 16, KUDAIWA KUBAKWA

Na Joseph Ngilisho, ARUSHA

HOFU imetanda katika eneo la Sanawari ya Juu, Moivo jijini Arusha baada ya kuibuka kundi la vijana kumbaka binti mwenye umri wa miaka 16 anayeishi na ulemavu wa akili, wakidaiwa kutumia nyumba isiyokuwa na makazi ya watu kutekeleza vitendo hivyo vya kinyama.

Tukio hilo limezua taharuki miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, huku familia ya mtoto huyo ikiiomba Serikali na Jeshi la Polisi kuwakamata haraka watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Baba wa binti huyo, Joseph Saitabahu, alisema tukio hilo liligundulika baada ya kumtilia shaka kijana mmoja aliyemuona akiingia katika nyumba inayodaiwa kuwa maficho ya vijana wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu.

Alisema aliporudi nyumbani hakumkuta mtoto wake, jambo lililomlazimu kurejea kwenye nyumba hiyo. Alidai alipofika alikuta mlango umefungwa, na baada ya kufunguliwa mtu mmoja alitoka akikimbia, hali iliyozidisha hofu kuwa kulikuwa na tukio la uhalifu lililokuwa limefanyika ndani.

"Nilimpeleka mtoto hospitalini kwa uchunguzi na madaktari walithibitisha kuwa alikuwa amefanyiwa ukatili wa kingono. Huo ulikuwa mshtuko mkubwa kwa familia yetu," alisema baba huyo kwa huzuni.

Alisema familia ilitoa taarifa katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central) Arusha na kupewa fomu ya PF3 kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu, lakini hadi sasa hakuna mtuhumiwa aliyekamatwa.

Kwa mujibu wa Joseph Saitabahu, anawafahamu baadhi ya vijana waliokuwa wakionekana mara kwa mara katika nyumba hiyo, akimtaja mmoja kwa jina la Salim, huku akidai nyumba hiyo imekuwa ikilalamikiwa na wananchi kwa muda mrefu kutokana na kutumiwa kufanyika vitendo vya uhalifu.

Naye baba mdogo wa mtoto huyo, Richard Saitabahu, alisema uchunguzi wa madaktari ulithibitisha kuwepo kwa dalili za ubakaji, huku akieleza kuwa familia inaendelea kuishi kwa hofu kutokana na watuhumiwa kutoweka mara baada ya tukio hilo.

"Tunaiomba Serikali na Jeshi la Polisi wawakamate wote waliohusika. Tunataka haki itendeke. Pia tunaomba nyumba hiyo ichunguzwe kwa kina kwa sababu imekuwa ikitajwa mara kwa mara na wananchi kuwa kitovu cha vitendo viovu," alisema.

Familia hiyo imeeleza kuwa mtoto huyo bado anaendelea na matibabu huku akikabiliwa na maumivu ya mwili na mshtuko mkubwa wa kisaikolojia uliotokana na tukio hilo.

Wakazi wa Sanawari ya Juu, Moivo wameiomba Serikali kuongeza doria za ulinzi na usalama pamoja na kuchukua hatua dhidi ya nyumba zinazodaiwa kutumiwa na wahalifu, wakisema hali hiyo imekuwa tishio kwa usalama wa watoto, wanawake na jamii kwa ujumla.

Hadi wakati habari hii inaandaliwa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha halikuwa limetoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo. Uchunguzi unaendelea ili kubaini ukweli wa madai hayo na kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kuhusika.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post