WATU WANANE WAFARIKI BAADA YA NDEGE YA KIJESHI YA MAREKANI KUANGUKA CALIFORNIA
By Arushadigital
Watu wanane, wakiwemo wafanyakazi wawili wa kampuni ya kutengeneza ndege ya Boeing, wamepoteza maisha baada ya ndege ya kijeshi aina ya B-52 Stratofortress ya Jeshi la Anga la Marekani kuanguka na kuwaka moto muda mfupi baada ya kupaa kutoka Kituo cha Jeshi la Anga cha Edwards kilichopo kusini mwa jimbo la California.
Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 11:20 jioni kwa saa za eneo husika (19:20 GMT) siku ya Jumatatu wakati ndege hiyo ikiwa katika misheni ya kawaida ya majaribio ya kiufundi.
Mashuhuda walieleza kuwa muda mfupi baada ya ndege hiyo kupaa, ilipoteza mwelekeo na kuanguka karibu na eneo la kambi hiyo, hali iliyosababisha mlipuko mkubwa na moshi mzito mweusi ulioonekana kwa umbali wa maili nyingi.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Kituo cha Jeshi la Anga cha Edwards, Kanali James Hayes, alisema taifa limepoteza watu muhimu waliokuwa wakihudumu katika sekta ya ulinzi na maendeleo ya teknolojia za kijeshi.
"Leo, Kituo cha Jeshi la Anga cha Edwards kimekumbwa na ajali mbaya na tumewapoteza Wamarekani wanane mashuhuri," alisema Kanali Hayes.
Aliongeza kuwa waliopoteza maisha ni mchanganyiko wa wanajeshi, wafanyakazi wa kiraia pamoja na wakandarasi wa serikali waliokuwa wakishiriki shughuli za kawaida za majaribio ya ndege hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka kituoni hapo, hakuna dalili za kuashiria kuwa mtu yeyote angeweza kunusurika kutokana na ukubwa wa ajali hiyo na moto uliotokea baada ya ndege kuanguka.
Kanali Hayes alisema taratibu za kuwataarifu ndugu na jamaa wa karibu wa marehemu zinaendelea, huku majina ya waliofariki yakitarajiwa kutangazwa rasmi baada ya kukamilika kwa mchakato huo ndani ya saa 24.
Kutokana na tukio hilo, shughuli katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Edwards zimesitishwa kwa muda wakati uchunguzi wa kina ukiendelea kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Ndege ya B-52 iliyohusika katika ajali hiyo ni moja ya ndege za kimkakati zinazotumiwa na Jeshi la Anga la Marekani, ikiwa imeboreshwa kwa mifumo ya kisasa ya rada na teknolojia nyingine za kijeshi. Hata hivyo, ilianguka muda mfupi baada ya kuondoka ardhini na kuwaka moto, hali iliyosababisha vifo vya watu wote waliokuwa ndani yake.
Maafisa wa usalama wa anga pamoja na wataalamu wa uchunguzi wa ajali za ndege wameanza kazi ya kukusanya ushahidi ili kubaini kilichosababisha ajali hiyo, ambayo imeibua mshtuko mkubwa ndani ya jeshi na sekta ya anga nchini Marekani.
Ends..

Post a Comment