WANAWAKE WAFANYABIASHARA WA SAMAKI WAFICHUA UNYANYASAJI WA KINGONO MWAMBAONI

WANAWAKE WAFANYABIASHARA WA SAMAKI WAFICHUA UNYANYASAJI WA KINGONO MWAMBAONI

Utafiti wa LHRC wabaini wanawake kulazimishwa kuingia mahusiano ili kupata samaki; mabadiliko ya tabianchi yatajwa kuongeza tatizo

Na Hadija Bagasha, Tanga

Wanawake wanaojishughulisha na biashara ya samaki katika mwambao wa Bahari ya Hindi wameibua tuhuma nzito za kukithiri kwa unyanyasaji wa kingono katika sekta hiyo, wakidai baadhi yao hulazimika kuingia katika mahusiano ya kimapenzi na wavuvi au manahodha wa vyombo vya uvuvi ili kupata samaki wa kuuza au kununua kwa bei nafuu.

Taarifa hizo zimeibuka kufuatia matokeo ya utafiti uliofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) katika mikoa ya Tanga, Lindi na Mtwara, uliolenga kuchunguza athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya uvuvi na haki za makundi yanayotegemea shughuli hizo kujipatia kipato.

Wanawake hao, ambao ni wanachama wa Umoja wa Wanawake Wavuvi wanaojihusisha na uchakataji, uanikaji, uchemshaji wa samaki pamoja na kilimo bahari, walisema vitendo hivyo vimeendelea kuwanyima haki ya kufanya biashara katika mazingira ya usawa, heshima na ushindani wa haki.


Mmoja wa wafanyabiashara hao, Rehema Juma, alisema wanawake wengi hulazimika kuvumilia mazingira ya udhalilishaji ili waweze kupata samaki kutoka kwa wavuvi au katika minada.

"Mimi kama mwanamke nikitaka kupata samaki sokoni au kwenye chombo cha mvuvi, mara nyingi natakiwa kuwa na mahusiano na mtu aliyepo kwenye chombo hicho. Huu ni unyanyasaji mkubwa tunaoupitia. Hata ukienda mnadani kununua samaki, unaweza kuongezewa dau makusudi ili ushindwe kununua na nafasi apewe mtu aliye kwenye mahusiano na muuzaji," alisema.

Kwa upande wake, Mwanakombo Ally alisema hata wanawake wenye uwezo wa kifedha hukosa fursa ya kupata samaki kutokana na upendeleo unaotolewa kwa wanawake walio katika mahusiano na baadhi ya wavuvi au manahodha.

"Wapo wanawake wenye fedha zao lakini wakifika bandarini au kwenye boti wanakuta samaki wamekwishaelekezwa kwa wengine walioko kwenye mahusiano na wavuvi. Hii ni aina ya ukatili wa kijinsia unaoendelea kutuumiza na kutunyima haki ya kufanya biashara," alisema.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo kwa wavuvi wa Moa, Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, Afisa wa Haki za Binadamu na Biashara wa LHRC, Clay Mwaifani, alisema utafiti umebaini uwepo wa vitendo vya ukatili wa kingono vinavyowakumba wanawake wanaofanya biashara ya samaki, hususan wachuuzi na wabebaji wa samaki maarufu kama "bodaboda wa samaki."

Alisema baadhi ya wanawake hulazimika kuingia katika mahusiano yasiyo ya hiari ili kupata upendeleo wa kununua samaki kwa bei nafuu au kupata bidhaa hizo kwa urahisi zaidi.

Mwaifani alisema changamoto hiyo imechangiwa pia na kupungua kwa upatikanaji wa samaki katika baadhi ya maeneo kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo imeongeza ushindani miongoni mwa wafanyabiashara.

"Kadiri samaki wanavyopungua, ushindani unavyoongezeka. Hali hiyo imewafanya baadhi ya watu kutumia nafasi zao vibaya na kusababisha wanawake kujikuta katika mazingira yanayotweza utu wao ili kuendelea kupata kipato," alisema.

Aliongeza kuwa LHRC imebaini baadhi ya wanawake wakikumbana na majina ya kudhalilisha, ubaguzi na shinikizo la kuingia katika mahusiano yasiyotokana na ridhaa yao kwa ajili ya kulinda maslahi yao ya kiuchumi.

Mbali na unyanyasaji wa kijinsia, utafiti huo umeonyesha kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanaendelea kuathiri uzalishaji wa samaki, jambo linalopunguza kipato cha wavuvi na wafanyabiashara wa samaki, hususan wanawake ambao wengi wao hutegemea sekta hiyo kuhudumia familia zao.

Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, Afisa Mkuu wa Uchunguzi wa LHRC, Chrisantus Ndibaiukao, alisema lengo la utafiti huo ni kuibua changamoto zinazowakabili wadau wa sekta ya uvuvi na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mazingira ya kazi pamoja na kulinda haki zao.

Alisema moja ya changamoto kubwa iliyobainika ni ushiriki mdogo wa wavuvi katika ngazi za maamuzi, jambo linalowafanya kushindwa kutetea maslahi yao na kushiriki kikamilifu katika mipango ya usimamizi wa rasilimali za bahari.

"Tunataka kuona sauti za wavuvi zikisikika zaidi katika michakato ya maamuzi ili sera na mipango inayowahusu izingatie mahitaji yao halisi na changamoto wanazokabiliana nazo kila siku," alisema.

Aidha, ripoti hiyo imebaini kuwa wanawake wengi katika sekta ya uvuvi wanakabiliwa na ukosefu wa mitaji, mazingira magumu ya kazi, ubaguzi wa kijinsia na vitendo vya unyanyasaji vinavyowadhoofisha kiuchumi na kijamii.

Utafiti huo pia umeonyesha kuwepo kwa migongano ya maslahi kati ya wavuvi wadogo na taasisi za uhifadhi wa mazingira ya bahari, ambapo jitihada za kulinda rasilimali za bahari zimekuwa zikipingana na mahitaji ya wananchi wanaotegemea uvuvi kama chanzo kikuu cha maisha yao.

Matokeo hayo yanaibua hitaji la hatua za haraka za kisera na kijamii ili kuhakikisha wanawake wanaofanya biashara ya samaki wanapata mazingira salama, yenye usawa na yanayolinda utu na haki zao za msingi huku wakishiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa buluu nchini.


Ends

Post a Comment

أحدث أقدم