MAMA AJIFUNGUA WATOTO WATANO KWA WAKATI MMOJA MUHIMBILI, HOSPITALI YAGHARAMIA MATIBABU YOTE
Na Arusha Digital | Dar es Salaam
Furaha na shangwe zimetawala kwa familia ya Victoria Mkwizu, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, baada ya kujifungua salama watoto watano kwa wakati mmoja katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Watoto hao walizaliwa Juni 13, 2026 na wanaendelea vizuri chini ya uangalizi maalumu wa wataalamu wa afya, huku watatu wakiwa wa kiume na wawili wa kike.
Akizungumza akiwa wodini, Victoria amesema ameridhishwa na huduma alizopatiwa tangu alipolazwa hadi kufanikisha kujifungua salama watoto hao watano, akieleza kuwa ushirikiano na uangalizi wa karibu kutoka kwa madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa afya umechangia mafanikio ya tukio hilo.
“Napenda kuwashukuru madaktari, wauguzi na watumishi wote wa Muhimbili kwa namna walivyonihudumia kwa upendo na weledi mkubwa katika kipindi chote cha matibabu hadi kujifungua salama watoto wangu,” amesema.
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa hospitali hiyo, Dk. Rachel Mhaville, amesema ujauzito wa watoto watano ni miongoni mwa ujauzito wenye hatari kubwa unaohitaji uangalizi wa karibu wa wataalamu wa afya kuanzia kipindi cha ujauzito hadi baada ya kujifungua.
Amesema kutokana na hali hiyo, hospitali iliunda timu maalumu ya wataalamu kutoka idara mbalimbali waliokuwa wakifuatilia maendeleo ya mama huyo ili kuhakikisha usalama wake pamoja na wa watoto.
“Ujauzito wa aina hii huhitaji maandalizi ya kina na usimamizi wa karibu wa wataalamu ili kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza kwa mama na watoto. Tunafurahi kuona wote wanaendelea vizuri,” amesema Dk. Mhaville.
Katika hatua ya kuonyesha dhamira ya kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi, Hospitali ya Taifa Muhimbili imetangaza kugharamia gharama zote za matibabu za Victoria na watoto wake kuanzia alipolazwa Mei 15, 2026 hadi watakapokamilisha matibabu na kuruhusiwa kurejea nyumbani.
Dk. Mhaville amesema uamuzi huo unalenga kuhakikisha mama na watoto wanaendelea kupata huduma stahiki na salama katika kipindi hiki muhimu cha uangalizi baada ya kujifungua.
Tukio hilo limeelezwa kuwa miongoni mwa matukio adimu ya uzazi yanayohitaji usimamizi wa hali ya juu wa kitabibu, huku likidhihirisha uwezo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili katika kushughulikia ujauzito na uzazi wenye changamoto kubwa kwa mafanikio.
Ends

إرسال تعليق