TRA YATOA MSAADA HOSPITALI YA BOMBO KUSAIDIA WATOTO NJITI KUELEKEA MIAKA 30 YAKE

 TRA YATOA MSAADA HOSPITALI YA BOMBO KUSAIDIA WATOTO NJITI KUELEKEA MIAKA 30 YAKE

Na Hadija Bagasha | Tanga

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa watoto wenye mahitaji maalum, hususan watoto njiti wanaopatiwa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo mkoani Tanga, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo.

Akikabidhi msaada huo, Naibu Kamishna wa Huduma za Kiufundi kutoka Makao Makuu ya TRA, Ted Silkiluwasha, alisema mamlaka imeamua kushiriki kusaidia makundi yenye uhitaji maalum kama njia ya kurudisha kwa jamii sehemu ya mchango unaotokana na kodi zinazolipwa na wananchi.

Alisema Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha maendeleo yanayochangiwa na mapato ya kodi yanawafikia Watanzania wote bila kumuacha mtu nyuma, hususan makundi yaliyo katika mazingira magumu.

“Sambamba na kuijenga Tanzania, hatupendi kumuacha mwananchi yeyote nyuma. Miaka 30 ya TRA imewezekana kutokana na walipa kodi, na mamlaka inatambua kuwa uhai wa walipa kodi ndio uhai wa TRA. Ndiyo maana tumeona ni muhimu kuwasaidia watoto njiti kama sehemu ya kurudisha kwa jamii,” alisema Silkiluwasha.

Aliongeza kuwa Julai 1 mwaka huu TRA itatimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake chini ya kaulimbiu ya “Tanzania kwa Pamoja Tunajenga Taifa Letu,” huku maadhimisho hayo yakiambatana na shughuli mbalimbali za kijamii nchini.

Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Castro John, alisema mamlaka hiyo inaamini kila Mtanzania ni mlipa kodi wa sasa au wa baadaye, hivyo watoto wanaopatiwa huduma leo ni sehemu ya kizazi kitakachochangia maendeleo ya taifa hapo baadaye.

Aidha, aliwataka wadau mbalimbali na taasisi za umma na binafsi kujitokeza kusaidia makundi yenye mahitaji maalum na kushiriki katika shughuli za kijamii zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya Hospitali ya Rufaa ya Bombo, Nuru Hamisi Omari alisema hospitali hiyo hupokea watoto njiti kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tanga kwa ajili ya matibabu na uangalizi maalum, ikiwemo huduma za kuongeza kiwango cha sukari mwilini na kusaidia kupumua kwa kutumia mashine maalum hadi wanapofikia uzito unaohitajika.

Naye Muuguzi Kiongozi wa Wodi ya Watoto, Sister Rukia Mbega, aliishukuru TRA kwa msaada huo uliowajumuisha sabuni, nepi, dawa na maziwa ya unga, akisema vifaa hivyo vitasaidia kuimarisha huduma na matunzo ya watoto njiti wanaopatiwa matibabu hospitalini hapo.






Ends

Post a Comment

أحدث أقدم