SIONI DHAMIRA YA DHAHIRI YA KUPATA KATIBA MPYA – KIBAMBA

 SIONI DHAMIRA YA DHAHIRI YA KUPATA KATIBA MPYA – KIBAMBA

Mwandishi Wetu, Dodoma

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Deus Kibamba, amesema haoni dhamira ya dhati kwa viongozi wa Serikali katika kuhakikisha Watanzania wanapata Katiba Mpya kwa wakati, akieleza kuwa mwelekeo wa sasa unaashiria msisitizo zaidi kwenye marekebisho badala ya mchakato wa kuandika Katiba mpya.


Akizungumza katika mjadala kuhusu fursa zilizopo kimataifa na kikanda katika nafasi za kiraia na ulinzi wa haki za binadamu, Kibamba alisema kauli zinazotolewa hivi karibuni zinaonyesha mwelekeo wa maboresho ya Katiba iliyopo badala ya mchakato mpana wa Katiba Mpya.

“Binafsi ukiniuliza kuhusu suala la kupata Katiba Mpya ambayo ndiyo msingi wa changamoto nyingi kwenye jamii, sioni dhamira ya dhati ya viongozi. Hivyo asasi za kiraia na wananchi lazima tuungane kuhakikisha tunapata Katiba Mpya,” alisema Kibamba.

Katika mjadala huo, wakili Jebra Kambole, wakili PraiseGod Joseph na James Marenga walibainisha kuwa bado kuna fursa ya kushirikiana na taasisi za kimataifa na kikanda katika kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa.

Wakili Kambole alieleza kuwa kesi za maslahi ya umma zilizowasilishwa mahakamani na baadhi yake kushinda zimekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uwajibikaji na kuendeleza utawala wa sheria nchini.

Kwa upande wake, wakili Marenga alisema kumekuwepo na jitihada mbalimbali za kisheria zinazolenga maboresho ya sheria, lakini changamoto kubwa ni kutotekelezwa kwa baadhi ya maamuzi ya mahakama na Serikali.

Mjadala huo kuhusu mikakati ya utetezi wa utawala wa sheria, nafasi ya kiraia na marekebisho ya sheria nchini Tanzania uliandaliwa na mashirika manne, yakiwemo Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Tanganyika Law Society (TLS), Zanzibar Female Lawyers Association (ZAFELA) na Pan African Lawyers Union (PALU).

Mashirika hayo yameendesha mjadala huo chini ya mradi wa Kulinda Utawala wa Sheria, Nafasi ya Kiraia na Uwajibikaji Tanzania kupitia ushirikiano na ubia ulioboreshwa (SCATZ), unaofadhiliwa na European Union.

Mjadala huo umehitimishwa kwa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya serikali, asasi za kiraia na wadau wa sheria ili kuendeleza utawala wa sheria na haki za binadamu nchini.

Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم